Saturday, November 8, 2014

AZAM FC YAZINDUKIA KWA COASTAL

Posted By: kj - 6:58 PM

Share

& Comment

AZAM FC imezinduka kutoka kwenye vichapo viwili mfululizo, baada ya kuilaza mabao 2-1 jioni hii Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche na beki Mtanzania, Shomary Salum Kapombe ndiyo waliofunga mabao hayo leo katika mchezo uliokuwa mkali na wa kusisimua.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Simon Mbelwa wa Pwani, Azam FC ndiyo waliokuwa wa kwanza kubisha hodi langoni mwa Coastal kupitia kwa mshambuliaji wake, Kipre Tchetche ambaye shuti lake liligonga mwamba akijaribu kuunganisha krosi ya Didier Kavumbangu.

Kipa Aishi Manula alifanya kazi ya ziada ya dakika ya saba baada ya kuokoa mchomo mkali wa mshambuliaji Mkenya, Rama Salim. Aishi tena alipangua shuti la Rama Salim aliyejaribu kuunganisha kona ya Joseph Mahundi dakika ya 12.

Azam FC ilipata bao lake la kwanza dakika ya 84, mfungaji Kipre Herman Tchetche aliyepokea pasi nzuri ya Mufathir Yahya na kutulia vizuri kabla ya kumchambua kipa Shaaban Kado.

Beki Shomary Kapombe aliifungia Azam FC bao la pili dakika ya 88 baada ya kupanda mwenyewe kwa kasi kutokea katikati ya Uwanja kabla ya kufika ndani ya boksi na kufumua shuti.

Rama Salim aliifungia Coastal Union bao la kufutuia machozi ya dakika ya 90 na ushei
Azam FC iliyofungwa mechi mbili mfululizo zilizopita 1-0 na JKT Ruvu na 1-0 na Ndanda FC, leo ilionyesha dhamira ya kushinda tangu mwanzo, japokuwa ilikutana na wapinzani wagumu.

Kwa ushindi huo, Azam FC inatimiza pointi 13 baada ya kucheza mechi saba, hivyo kurudi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, mbele ya Yanga SC yenye pointi 13 pia.

Coastal Union inashuka kwa nafasi mbili hadi ya nne ikibaki na pointi zake 11.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao/Leonel Saint-Preux dk67, Mudathir Yahya, Didier Kavumbagu/Gaudence Mwaikimba dk82, Sure Boy na Kipre Tchetche.

Coatsal Union; Shaaban Kado, Mbwana Hamisi Kibacha ‘Radebe’, Sabri Rashid, Abdallah Mfuko/Yussuf Chuma dk30, Tumba Sued, Mohamed Shekuwe/Razack Khakfan dk51, Kenneth Masumbuko, Joseph Mahundi, Bright Obinna, Rama Salim na Itumbi Imbem.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.