Thursday, November 20, 2014

FATHER: MORAD YUMO KWENYE MIPANGO YA TIMU, WANAO MUHITAJI TCHECHE HAWAJAREJESHA JAWABU

Posted By: kj - 5:59 PM

Share

& Comment

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM

AZAM FC wamewaambia wazi, Simba SC kwamba hawawezi kumpata beki Said Mourad.
Simba SC walifanya mazungumzo na Azam FC kumuomba Mourad, lakini wakajibiwa kwamba mlinzi huyo wa kati yupo katika mipango ya muda mrefu ya klabu hiyo.

Katibu wa Azam FC, Nassor Idrisa Mohammed ‘Father’ ameiambia BIN ZUBEIRY mchana wa leo kwamba, pamoja na kusajiliwa kwa Serge Wawa Pascal, lakini Mourad haondoki.

“Ukweli ni kwamba Simba SC walifanya mazungumzo na sisi, yasiyo rasmi lakini wakisema wanamtaka Mourad, ila tukawaambia wazi huyo mchezaji yupo kwenye mipango yetu ya muda mrefu,”amesema Father.
Azam FC wamekataa kuwauzia Simba SC beki Said Mourad

Kwa ujumla, Father amesema hakuna beki yoyote wa kati wa Azam FC atakayeachwa kwa sababu ya kusajiliwa mlinzi kutoka Ivory Coast, Serge Wawa aliyekuwa anachezea El Merreikh ya Sudan.

“Aggrey Morris, David Mwantika na Mourad wote wataendelea kuwa wachezaji wa Azam FC kwa pamoja na Wawa. Tena inakaa vizuri tu, unakuwa na walinzi wawili ndani, wengine wa akiba,”amesema.

Nassor amesema kwamba ni salama sana kuwa na wachezaji zaidi ya mmoja katika nafasi muhimu kama hizo, hata ikitokea bahati mbaya ya majeruhi au mtu kupewa kadi, wanakuwepo wa kuziba nafasi zao.

Kuhusu mshambuliaji wao, Kipre Herman Tchetche anayetakiwa na klabu ya Kelantan FC ya Malaysia, Katibu huyo wa Azam FC amesema; “Jamaa walituma mambo ya kumtaka huyu mchezaji, tukawajibu na kuwapa dau ambalo tunataka, lakini wamekuwa kimya hadi sasa,”.
Dili la Kipre Tchetche kwenda Malaysia limepatwa ukakasi

Father amesema Kipre bado yupo Azam FC na ana Mkataba wa miaka miwili, hivyo huyo ni mchezaji wao halali hadi hapo klabu hiyo inayomtaka itakapomalizana nao.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wanatarajiwa kuanza mazoezi wiki ijayo baada ya mapumziko mafupi kufuatia kusimama kwa ligi hiyo wiki mbili zilizopita iliyopita.

Ligi Kuu ilisimama baada ya mechi za Novemba 9 na inatarajiwa kutejea tena Desemba 26, mwaka huu. 


CHANZO: BIN ZUBEIRY 

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.