Tuesday, December 30, 2014

OMOG: TUTAHAKIKISHA TUNASHINDA KILA MCHEZO

Posted By: Unknown - 7:23 AM

Share

& Comment

KOCHA wa Azam Fc, Joseph Omog amesema ni mapema kukata tamaa ya kutetea taji la Ligi Kuu kwa vile bado ligi ni ndefu na kwamba kuna uwezekano wa kuendelea kutetea taji hilo.

Akizungumza juzi baada ya mechi yao dhidi ya Yanga iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kutoka sare ya mabao 2-2, Omog alisema hawawezi kukata tamaa kwa kuwa wamejipanga kuendelea kuwa bingwa kwa msimu huu.

Alisema wanaendelea kurekebisha mapungufu na taratibu kiwango chao kitarudi kama zamani.

"Tunajaribu taratibu tutarudi katika kiwango chetu, ligi ni ndefu kuna uwezekano wa kutetea taji," alisema na kuongeza kuwa matarajio yao ni kushinda kwa kila mchezo.

Akizungumzia mchezo wao na Yanga juzi, alisema matokeo ya sare waliopata sio mabaya kwani ni sehemu ya mchezo. Alisema mechi ile ilikuwa baina ya timu mbili kubwa na zilicheza mchezo mzuri na kinachohitajika kwao ni kuendelea na mapambano.

Omog ndiye aliyeipa timu hiyo ubingwa msimu uliopita ambapo alisema atafurahi kama wataendelea kushikilia taji hilo kwa msimu mwingine.

Kikosi hicho kinatarajiwa kuwakaribisha Mtibwa Sugar katika uwanja wao wa nyumbani mwishoni mwa wiki hii. Timu zote mbili zinakimbizana kwa pointi ambapo Mtibwa Sugar ikiwa na pointi 16, Azam wana pointi 14.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.