
KOCHA wa Azam FC, Joseph Omog ametamba kuonesha ubora waliokuwa nao kwa kuisambaratisha Mtibwa Sugar, katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar.
Omog alisema pamoja na kikosi chake kupata ushindi mdogo wa bao 1-0 katika mechi mbili za hatua ya makundi, lakini ana kikosi bora kushinda cha wapinzani wao Mtibwa na atadhihirisha hilo kwa kuitoa timu hiyo inayoongoza Ligi Kuu ya Tanzania bara.
“Watu wengi wametutoa kwenye mbio za ubingwa mwaka huu, kwa sababu tumekuwa tukipata ushindi mdogo katika mechi za makundi, lakini hiyo siyo sababu tuna kikosi kikubwa na bora ambacho kina uwezo wa kucheza na timu yoyote inayoshiriki michuano hiyo na kupata ushindi na hilo tutalidhihirisha kwa Mtibwa,” alisema Omog.
Omog alisema kwa jinsi ambavyo ana kikosi kikubwa hadi sasa kuna wachezaji ambao hajawatumia hata mechi moja ya mashindano hayo, ambao ni Kipre Tchetche na pacha wake Michael Bolou anaotarajia kuanza kuwatumia leo.
“Hawa ni wachezaji muhimu kwenye kikosi changu na sijawatumia tangu tufike hapa, lengo langu ni kuweka nguvu kubwa kuanzia hatua hii ya robo fainali, kwa sababu najua timu nyingi zimejiandaa na lengo langu ni kuchukua ubingwa ili kuweka rekodi nyingine,” alisema Omog.
Katika mechi za makundi, Azam imeshinda mechi mbili dhidi ya KMKM na Mtende Rangers na iliweza kutoka sare ya mabao 2-2 na mabingwa watetezi waliomaliza vinara kwenye kundi hilo KCCA ya Uganda siku ya ufunguzi.
CHANZO: HABARI LEO
0 Maoni:
Post a Comment