Monday, February 9, 2015

AGGREY AMEFUNGA KITANZI KINGINE

Posted By: kj - 12:44 PM

Share

& Comment

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh5NKi7NeNJd79PHg467EFNsg2JoYiFGNVWgDZ_cVDlKHl9XoRVadNcH99XHLuiZhif980mrqPCpYoxGccq16NzdhtWcWMWJiKubQWBlnU9X7V6VYbCBPOtZUltq1euE7XagYtroHYHeaM/s1600/aggrey+morris.jpg
Na Edo Kumwembe, Mwanaspoti
 
AGGREY Morris amepigwa jela ya mechi tatu za soka. Ni kutokana na ushahidi wa moja kwa moja kupitia kituo cha televisheni cha Azam TV ambayo wamiliki wake ni wale wale wa timu yake Azam FC. Haki imetendeka.

Mwamuzi hakuona. Waamuzi wasaidizi hawakuona. Mwamuzi wa mezani hakuona. Kamera ziliona. Ni ushindi kwa teknolojia. Labda ni mwanzo wa zama mpya.

Kwa nini Aggrey alifungiwa? Aggrey hakuwa katika nafasi ya kuucheza mpira. Asingeweza kukabiliana na kasi ya Emmanuel Okwi, ambaye alikuwa anaingia katika eneo la hatari kwa staili ya kucheza ‘One two’ na Simon Sserenkuma.

Ingawa mpira ulikuwa kwa Sserenkuma ambaye hakuwa na nia tena ya kumpasia Okwi, Agrey alijua kwamba kama Mganda huyo angeamua kumrudishia mpira Mganda mwenzake Okwi, basi asingeweza kumzuia kutokana na kasi ya Okwi katika kuingia ndani ya eneo la hatari.

Kwa kugundua hilo, Aggrey alimkinga kwa kiwiko Okwi ambaye alikuwa hatazami njia yake. Ilikuwa ni faulo ya wazi ambayo katika soka huwa tunaita ‘Obstruction’. Bahati mbaya kwa Aggrey ni kwamba Okwi alipoteza fahamu.

Wakati mwingine siyo kila mchezaji anaweza kupoteza fahamu kwa pigo lile. Tatizo pekee kutoka kwa wanasiasa waliopo katika soka, ni ukweli kwamba baadhi yao walianza kupotosha ukweli na kuamua kuongeza chumvi kwa kudai kuwa, Aggrey alikuwa amedhamiria kumzimisha OKwi. Siyo kweli. Alidhamiria kumzuia kiuhuni. Kuzimia au kutozimia ni matokeo ya pigo lenyewe.

Kwa kuwa mwamuzi hakuona, wasaidizi wake hawakuona, wala mwamuzi wa mezani hakuona, kwa wenzetu kule Ulaya wanachofanya ni kupitia mkanda wa televisheni na kumuuliza mwamuzi angefanya nini kama angeona tukio lile.

Kama mwamuzi anasema angetoa kadi ya njano, Aggrey asingefungiwa. Kama mwamuzi angesema angetoa kadi nyekundu, basi adhabu ya Agrey ni sawa kabisa na anastahili kufungiwa mechi tatu. Naamini kamati iliyomfungia Aggrey ilifanya hivyo kwa sababu hata mimi ningetoa kadi ya nyekundu kwa Aggrey.

Hata hivyo, nina matatizo mawili katika hili. Je, huu ni mwendelezo mpya wa baadhi ya kanuni zetu za soka. Katika siku za karibuni baada ya kupigwa kwa Okwi na mshambuliaji wa Yanga, Amiss Tambwe, kumekuwa na kelele nyingi katika vyombo vya habari kuhusu ubabe waliofanyiwa.

Hata hivyo, ukirudisha nyakati nyuma, miaka michache iliyopita, walinzi wa Yanga na Simba walikuwa wanatembeza ubabe kama huu lakini hakuna aliyejali. Rafiki zangu, Juma Nyosso na Kevin Yondani walijulikana kwa ubabe huu wakiwa katika jezi za njano na kijani. Tupo tayari kuona kanuni hii inafuatwa tena na tena?

Kanuni hii ikiendelea kufuatwa tena na tena itatusaidia sana. Pia itaanza kuleta shida katika siku za usoni kwa sababu ni rahisi kusema Azam TV inazihujumu Simba na Yanga kwa ajili ya kuisaidia Azam FC. Tukio la Agrey liwekwe katika kumbukumbu kwa ajili ya kutenda haki siku za usoni.

Hata hivyo, tatizo langu jingine linatokana na tatizo la kwanza. Ukiangalia marudio yote ya ujinga wa Aggrey, pia yanatokana na ujinga wa mwamuzi msaidizi wa upande wa Mashariki ambaye aliruhusu Okwi aucheze mpira ambao umetoka kabisa.

Picha za marudio zinamwonyesha kiungo wa Azam, Mudathir Mudathir akiondoka kwa kutembea taratibu kuiruhusu timu yake irushe mpira. Ghafla Okwi akauchukua mpira ulio nje na kuuingiza ndani na kwenda katika lango la Azam.

Kwa nini yule mwamuzi msaidizi hajasimamishwa kwa kushindwa kumsaidia mwamuzi wa mechi? Kwa nini tumeanzia kuliangalia tukio katika vurumai ya Agrey na Okwi? Jibu ni moja tu. Ni kwa sababu baada ya kuzimia kwa Okwi, kelele nyingi zilitoka upande wa Simba juu ya Aggrey.

Walioamua kuhusu kufungiwa kwa Agrey walikuwa sahihi, lakini walimezwa na presha ya kelele tu bila ya kuzingatia kuwa uamuzi wowote ambao wangeuchukua, unafungua ukurasa wa uamuzi mwingine katika siku za usoni.

Pia, hata hili la mwamuzi msaidizi halijachukuliwa kwa umakini mkubwa kwa sababu mwamuzi msaidizi hana jina kubwa na si staa. Lakini kwa nini matukio kadhaa yanayopendelea timu kubwa yananaswa vizuri katika televisheni na kutolewa uamuzi kuliko yale ya timu ndogo?

Mwamuzi wa pambano la Yanga dhidi ya Mgambo Uwanja wa Taifa alivurunda. Aliinyima Mgambo penalti ya wazi na hapo hapo akaamua kumzawadia kadi ya njano ya kichekesho mshambuliaji wa Mgambo aliyedaiwa kujirusha. Kwa nini Mwamuzi yule hajafungiwa mpaka leo? Ni kitu cha kushangaza.

Hata hivyo, mwamuzi wa Yanga na Ruvu Shooting ameshafungiwa tayari. Ni kwa sababu Yanga wana kelele za kusikika kuliko Mgambo. Tuanze kuwa makini na uamuzi wa televisheni. Tusiuangalie kwa jicho la kengeza. Tutaona mengi raundi ya pili itakapowadia, lakini tunaweza kujikuta tunaumbuka wenyewe pindi tutakapofikiria tukio la Aggrey.

Aggrey alistahili kufungiwa, lakini tusije kuwasahau wengine wengi watakaostahili kufungiwa siku za usoni!

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.