
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC wametamba kuendeleza vipigo vyao dhidi ya timu ngumu kufungika nyumbani ya Ruvu Shooting mkoani Pwani kesho.
Mechi hiyo ilipaswa kuchezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini ikapigwa kalenda na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na ushiriki wa Azam FC katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwaka huu.
Jaffar Idd Maganga, msemaji wa Azam FC, ameuambia mtandao huu jijini hapa muda mfupi uliopita kuwa kikosi chao kilichozitandika 5-2 Mtibwa Sugar na 2-0 El-Merrikh katika mechi mbili zilizopita, kiko tayari kuendeleza ubabe dhidi ya timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
“Tunatambua Ruvu ni wagumu kufungika kwenye uwanja wao wa nyumbani, lakini tumejipanga vyema kwa ajili ya mechi zote msimu huu,” amesema Maganga.
Azam FC inayonolewa na Mcameroon Joseph Omog, ndiyo timu pekee ya nje ya mkoa wa Pwani iliyofanikiwa kuifunga Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini msimu uliopita, wakiichapa mabao 3-0.
Kikosi cha Mkenya Tom Alex Olaba cha Ruvu Shooting kimepoteza mechi moja tu kwenye uwanja huo msimu huu, kikifumuliwa 2-0 dhidi ya timu ‘kibonde’ katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Tanzania Prisons Septemba 20, mwaka jana.
Wanalambalamba wanaongoza msimamo wa ligi wakiwa na pointi 25 sawa na Yanga walioko nafasi ya pili, wakati Ruvu Shooting wako nafasi ya sita wakiwa na pointi 19 sawa na Mtibwa Sugar katika nafasi ya tano, Coastal Union (7), JKT Ruvu (8) na Polisi Moro (9).
Ruvu Shooting iliyofungwa 2-0 dhidi ya Azam FC mzunguko wa kwanza Uwanja wa Azam jijini hapa Septemba 27, mwaka jana, itaingia uwanjani kesho ikiwa na kumbukumbu ya kushinda 2-1 katika mechi zake mbili za nyumbani zilizopita dhidi ya Mtibwa Sugar na Stand United.
0 Maoni:
Post a Comment