Thursday, September 3, 2015

AME ALLY: MAXIMO ALINIKATAA YANGA

Posted By: kj - 4:37 PM

Share

& Comment

Amme Ally 'Zungu'
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam (www.shaffihdauda.co.tz)

Mshambulizi wa Azam FC, Ame Ally ‘Zungu’ amefanya mahojiano marefu na mtandao huu na kuelezea historia yake ya uchezaji. Hakika wachezaji wengi wa Kitanzania wamekutana na changamoto nyingi kabla ya kupata umaarufu. Ame alipumzika kucheza mpira kwa vipindi viwili tofauti kutokana na hali ya kimaisha lakini mchezaji huyo aliyeanza kucheza ligi kuu bara msimu uliopita alianza maisha yake ya mpira wa ushindani katika klabu ya Duma FC ya Pemba mwaka 2010.

Alicheza kwa misimu miwili kisha akapumzika kucheza mpira kwa mwaka mmoja kabla ya kurejea tena uwanjani na kujiunga na timu ya Chuoni FC ambayo aliichezea hadi aliposajiliwa na Mtibwa katikati ya mwaka 2014.

“Nilikutana na changamoto za mpira ndiyo maana kuna wakati nilipumzika kucheza mpira. Unaweza ukawa unacheza mpira lakini mwisho wa siku maisha yanaendelea kuwa magumu. Niliacha kwa muda na kugeukia upande mwingine ili kukabiliana na maisha lakini huko pia mambo yalikuwa magumu zaidi nikaamua kurudi tena katika mpira mwaka 2013 baada ya kuona nina nguvu”.

Anaanza kusema straika huyo aliyefanya vizuri msimu uliopita akiwa Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro. Ame amecheza ligi daraja la Pili Zanzibar mwaka 2007 kisha akapumzika kwa mwaka mmoja na kujiunga na timu ya daraja la kwanza mwaka 2009. Alichezea Duma kisha Chuoni kabla ya kuja Dar es Salaam kujaribu maisha ya mpira. Alikwenda Simba SC lakini akapelekwa timu ya pili ( Simba B) kwa majaribio mwaka uliopita.

www.shaffihdauda.co.tz: Ilikuwaje ukaja bara?

AME ALLY:  Mwaka 2013 nilipokuwa Chuoni FC tulimaliza katika nafasi ya pili ya ligi kuu ya Zanzibar. Kuna Mzee mmoja alikuja akaniambia ‘wewe uwezo unao, njoo ubahatishe na huku (Tanzania bara) nikamwambia si tatizo, lakini ngoja kwanza nijipange nijue nitafanye.

Kweli baada ya muda niliamua kuondoka Chuoni nikaja Dar. Nilipofika akaniambia ‘nenda katika timu fulani fulani ukajaribu tuangalie itakuwaje’. Nilienda Simba pale nikafanya majaribio. Sikwenda moja kwa moja katika timu ya kwanza bali nilipelekwa katika timu B. Nilifanya pale kwa siku kadhaa lakini nikajiambia mwenyewe kiwango changu si cha kucheza timu B. Nikasema siwezi kucheza timu B nikaondoka.

Baada ya kuondoka pale kuna mtu mmoja akaniambia unaweza kwenda kufanya majaribio Yanga SC. Nikamwambia si mbaya lakini kipindi kile nilichotakiwa kwenda kufanya majaribio Yanga kwa bahati mbaya akaja Marcio Maximo (mwalimu wa Yanga). Maximo alisema hahitaji mchezaji ambaye atakuja kufanya majaribio bali anahitaji wachezaji ambao walisajiliwa kwa hiyo sikupata nafasi ya kufanya majaribio Yanga.

www.shaffihdauda.co.tz: Baada ya kuachana na Simba B na Maximo kufunga milango kwa wachezaji wa majaribio. Nini kiliendelea?.

AME ALLY: Kabla sijaenda Mtibwa nilienda katika uwanja mmoja hivi unaitwa Garden upo pale Kinondoni. Nilifanya mazoezi kama miezi miwili. Nilikuwa naenda kufanya mazoezi pale (Kinondoni) halafu nakaa Mbagala, niliendelea kufanya mazoezi pale huku nikiwa bado sijapata timu.

www.shaffihdauda.co.tz: Ilikuwaje ukaenda Mtibwa?

AME ALLY: Unajua pale Garden kuna watu wengi sana wanacheza, kwa mfano ligi ikiwa imesimama au imemalizika pale huwa kuna wachezaji wengi maarufu. Nilibahatika kucheza na Shaaban Nditti (nahodha wa Mtibwa Sugar) katika mazoezi ya pale. Nikamwambia ‘Shaaban unaweza kunisaidia kupata nafasi Mtibwa’. Akaniambia ‘subiri tucheki’.

www.shaffihdauda.co.tz: Ilichukua muda gani baada ya Shaaban kukwambia hivyo?

AME ALLY: Ilichukua karibu mwezi mmoja na nusu kwa sababu kuingia kule (Mtibwa) ilikuwa ngumu kwa sababu nilikuwa na mkataba na Chuoni kwa sababu Mtibwa hivi karibuni inasaini wachezaji  wengi wasio na mikataba. Nikamwambia Shaaban hiyo haitakuwa ngumu sana nitajua mimi nitakachokifanya ili mradi mimi nije tu kucheza ligi kuu bara.

www.shaffihdauda.co.tz: Kitu gani kilitokea hadi tukakuona Mtibwa msimu uliopita tena kwa mafanikio?

 AME ALLY: Kwa ufupi tu ni maelewano tu baina ya Chuoni na Mtibwa. Uongozi wao walielewana ikawa freshi tu na mimi mwenyewe nilikubali.

www.shaffihdauda.co.tz: Baada ya msimu wa kwanza wa mafanikio katika ligi ya bara, unaingia msimu wa pili ukiwa katika moja ya klabu iliyotwaa ubingwa katika miaka miwili iliyopita, umejipangaje?

AME ALLY: Mpira una changamoto nyingi na malengo yangu si kufika Azam FC ndio niridhike, hapana, nataka nifike mbali zaidi ya hapa nilipo. Macho yangu kwa sasa si hapa tena.

www.shaffihdauda.co.tz: Kuna tofauti gani kati ya Mtibwa na Azam?

 AME ALLY: Ukiweka Azam na Mtibwa karibu asilimia 90 ya wachezaji nchini wataichagua Azam FC. Mchezaji wa Kitanzania ukimwambia twende Azam hawezi kurudi nyuma si kwamba ataikataa na Mtibwa, hapana lakini kwanza ataichagua Azam.

www.shaffihdauda.co.tz: Changamoto gani ambazo umekutana nazo katika maisha ya mpira?

AME ALLY: Changamoto ni nyingi, mfano, kule Zenji (Zanzibar) nilikuwa naenda mazoezini bila nauli. Unawezaje? Au unachezaje mpira? Unakosa hata shilingi 100!. Unakwenda mazoezi lakini unarudi nyumbani huna hata shilingi 2000 ‘mtu una familia’. Kama wewe utakula nini?

www.shaffihdauda.co.tz: Lazima uwe katika wakati mgumu.

AME ALLY: Wakati mwingine hata viatu, unakuwa huna hata hela ya kununulia viatu vya kuchezea. Timu inatoa pea moja ya viatu, hivyo hivyo vinatumika katika mechi na mazoezi ama wakati mwingine hawatoi kabisa hivyo mchezaji unapaswa kujinunulia.

Muda wa kutafuta hela unakuwa hakuna kwa sababu kazi yako ni mpira na muda mwingi unatumia kucheza mpira. Kwa maana hiyo hata uwezo wa kununua pea ya pili ya kiatu unakuwa huna kwa sababu hakuna njia nyingine ya kuingiza hela nje ya mpira.

www.shaffihdauda.co.tz:  Kwa kawaida wachezaji wetu wengi wanapitia hali hiyo.

AME ALLY: Kweli, kweli kabisa, yaani naenda kucheza mechi kwa kiatu cha kuazima. Kweli mchezaji unaazima kiatu?. Kweli unaipenda kazi lakini unakutana na mazingira yaliyo magumu kimaisha. Hela ya chakula yenyewe inakuwa tatizo. Haiwezekani nimepata 20,000 nikanunue kiatu wakati nina familia.

www.shaffihdauda.co.tz: Watu wengi wanawachukulia wachezaji wa Zanzibar kama ‘ wasio na nguvu’ lakini hivi sasa ukitazama katika klabu zetu kubwa wamejaa wachezaji kutoka Visiwani, hii ina maanisha nini? Ni kweli hamna nguvu au ‘ kasumba’ yetu iliyozoeleka?.

AME ALLY: Nikwambie ukweli, unajua sisi kule kwetu Zanzibar tunajua sana mpira kuliko watu wa bara. Nielewe kwanza navyokwambia, ila sisi kule tunacheza zaidi ‘ total football-mchezo wa kushambulia na kuzuia kwa pamoja huku timu ikipasiana sana’.

Sisi tunacheza zaidi mpira na kuweka nguvu za wastani lakini wachezaji wa bara wanatumia sana nguvu. Sisi hatuchezi ‘ mpira wa mwilini’ tunapiga pasi hivyo si rahisi kuwangia mwilini. Bara wanatumia sana nguvu lakini sisi tunacheza mpira wa kawaida, tuseme kama mpira wa FC Barcelona ya Hispania. Kuhusu nguvu hilo ni jambo la mchezaji mwenyewe kwa sababu ya vile utakavyojiweka wewe mwenyewe.

www.shaffihdauda.co.tz: Uliwezaje kuwa mudu walinzi wenye nguvu katika msimu wako wa kwanza Bara?.

AME ALLY: Kwanza, Ilibidi nitumie nguvu, kwa sababu nilishafahamu stahili ya mabeki wengi wa huku. Pili, nilijua kabisa hapa bila kutumia nguvu za ziada hauwezi kufanya vizuri.

 Nilishacheza na mabeki karibu watatu au wanne alafu ‘mabubu’ hawaongei na shughuli yao Mungu mwenyewe anajua kwa hiyo kwangu mimi sina hofu na beki wa aina yoyote kwa sababu Mungu amenijalia nina nguvu zangu mwenyewe, amenijali ‘umbo’ nashukuru Mungu muda wowote mimi napambana.

www.shaffihdauda.co.tz: Ulianza kwa kasi msimu uliopita lakini ghafla, Ame Ally akawa hafungi magoli.

AME ALLY: Hali hiyo ilichangiwa na kucheza mfululizo kwa sababu kule kwetu Zanzibar hakuna wingi wa mashindano. Tulitoka kwenye ligi na kuingia katika Mapinduzi Cup pia ligi ya bara ina timu nyingi na ngumu tofauti na Zanzibar. Vilevile timu ilikuja kupotea kiujumla hivyo kuna vitu vingi vilikosekana na mawazo kuhusu maisha ya Mtibwa yalichangia kushuka kwa kiwango changu.

www.shaffihdauda.co.tz: John Bocco, Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche, Allan Wanga unazungumziaje ushindani wa namba katika timu ya Azam FC.

AME ALL: Wale tayari wameshacheza mashindano makubwa, jambo la msingi ni mimi mwenyewe kujifua ili kumshawishi mwalimu anipe nafasi.

0714 08 43 08

Shukrani kwa: www.shaffihdauda.co.tz

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.