Tuesday, October 27, 2015

MKWASA AMREJESHA SURE BOY TAIFA STARS

Posted By: kj - 8:10 PM

Share

& Comment

Kiungo wa Azam FC Salum Abubakari "Sure Boy katika mchezo dhidi ya Mbeya city msimu huu katika uwanja wa Azam complex Chamanzi
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa, amemrejesha kikosini kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’.


Kikosi hicho kipya cha wachezaji 28 alichokitangaza leo ni mahususi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa raundi ya pili ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi dhidi ya Algeria ‘The Desert Foxes’.

Mchezo wa kwanza utafanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Novemba 14 kabla ya wa marudiano kupigwa jijini Algiers Novemba 17, mwaka huu.

Mara ya mwisho Sure Boy kuichezea Stars ilikuwa ni kwenye michuano ya Kombe la Cosafa iliyofanyika Mei mwaka huu nchini Afrika Kusini na Stars kutolewa katika hatua ya makundi bila pointi yoyote.

Wakati huo Stars ilikuwa ikinolewa na Mholanzi Mart Nooij, aliyetimuliwa kwa matokeo mabaya ya kikosi hicho kwenye mechi za michuano mbalimbali na nafasi yake hivi sasa imechukuliwa na Mkwasa.

Jumla ya wachezaji nane wa Azam FC wameitwa kwenye kikosi hicho, idadi inayolingana na wale wa Yanga SC waliojumuishwa.

Nyota wengine wa Azam FC walioitwa ni mmoja wa makipa bora nchini kwa sasa anayechipukia Aishi Manula, beki kisiki wa kulia Shomari Kapombe, nahodha wa kikosi hicho John Bocco, winga teleza Farid Maliki, viungo wabunifu Himid Mao, Frank Domayo na Mudathir Yahya.

Mkwasa pia amewaita wachezaji wengine wapya, ambao ni kinara wa ufungaji mabao kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Elias Maguli (Stand United) mwenye mabao nane, mshambuliaji Malimi Busungu (Yanga), beki wa kulia Hassan Kessy (Simba), beki wa kati Salim Mbonde (Mtibwa Sugar).

Kikosi kamili kinaundwa na makipa Aishi Manula (Azam FC), Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).

Mabeki ni Shomary Kapombe (Azam FC), Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (C), Kelvin Yondan (Yanga), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka (Simba) na Salim Mbonde (Mtibwa Sugar).

Viungo ni Himid Mao, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo (Azam), Jonas Mkude, Said Ndemla (Simba) na Salum Telela (Yanga).

Washambuliaji ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngassa (Free State Stars, A. Kusini), Farid Maliki, John Bocco (Azam), Simon Msuva, Malimi Busungu (Yanga ), Elius Maguri (Ruvu Shooting) na Ibrahim Ajibu (Simba).

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.