Msimu uliopita Azam FC ilikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Ndanda kwenye uwanja huo, lakini ikajibu mapigo kwa kuipiga kipigo kama hicho waliporudiana Uwanja wa Azam Complex.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Dennis Kitambi, aliuambia mtandao huu kuwa timu itaondoka jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani Mtwara leo saa 5 asubuhi mara baada ya mazoezi.
“Tunajua Ndanda itaingia uwanjani ikitaka kuendeleza kututambia, lakini sisi tumejipanga kukabiliana nao, kikubwa tunafikiria ushindi tu ili kuendelea na mwenendo wetu mzuri tulioenda nao,” alisema.
Kitambi atayeingia kwenye mchezo huo kwa kucheza dhidi ya timu yake hiyo ya zamani, alisema mpaka sasa kikosi cha Azam FC kiko safi na kudai kuwa hadi kufikia leo jioni benchi la ufundi litajua ni wachezaji gani hawapo fiti kwa kipute hicho.
Timu zote zilitoka sare kwenye mechi zao zilizopita, Azam FC ikipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga kwenye mechi iliyogubikwa na maamuzi ya utata na mwamuzi Abdallah Kambuzi huku Ndanda ikitoka suluhu walipoikaribisha Toto Africans ya Mwanza.
Azam imeanza vema kibarua cha kusaka taji hilo la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) mpaka sasa ikikabana koo na mpinzani wake Yanga, wote wakiwa na pointi 16, lakini inazidiwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
0 Maoni:
Post a Comment