Saturday, October 24, 2015

WACHEZAJI KUPEWA MAPUMZIKO BAADA YA TIZI LA LEO COCO BEACH

Posted By: kj - 7:18 AM

Share

& Comment


TIMU ya Azam FC imerejea jana saa 7 mchana jijini Dar es Salaam ikitokea mkoani Mtwara ilipoichapa Ndanda bao 1-0, huku kikosi hicho kikitarajia kufanya mazoezi yake kwenye fukwe za Coco Beach leo saa 2 asubuhi.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ilipata ushindi huo kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani humo.

Bao pekee la Azam FC kwenye mchezo huo lilifungwa na beki wa kulia Shomari Kapombe kwa kichwa safi, akiunganisha krosi safi ya Kipre Tchetche.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffary Idd, aliuambia mtandao huu kuwa mara baada ya mazoezi hayo ya ufukweni, wachezaji watapewa mapumziko ya siku moja kwa ajili ya kwenda kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa Taifa kesho.

"Kila mtu ana haki ya kupiga kura, hivyo sisi kama Azam FC tunalichukulia kwa uzito suala hilo, ndio maana tumewapa uhuru wachezaji wakatimize haki yao hiyo, tunategemea mara baada ya tukio hilo, timu itarejea tena mazoezini Jumatatu ijayo," alisema.

Azam FC inatarajia kushuka tena dimbani Alhamisi ijayo kuvaana na maafande wa JKT Ruvu, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Wakati Azam ikijikusanyia jumla ya pointi 19 sawa na Yanga iliyokuwa kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, JKT Ruvu bado haijawa na mwenendo mzuri kwenye ligi ikiwa mkiani katika msimamo wa ligi ikivuna pointi mbili tu ndani ya mechi nane walizocheza.

Katika kujiondoa kwenye hali hiyo mbaya, uongozi wa JKT Ruvu umeliongezea nguvu benchi lake la ufundi kwa kumchukua kocha mkongwe nchini Abdallah Kibadeni 'King' baada ya Fred Minziro kujiuzulu.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.