TIMU ya Azam FC imeendeleza wimbi la kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuichapa Ndanda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona leo.
Bao pekee la Azam FC limefungwa na beki wa kulia Shomari Kapombe dakika ya 79 kwa kichwa safi kilichomshinda kipa wa Ndanda, Jackson Chove.
Azam iliyotengeneza takribani nafasi 12 kwenye mchezo huo, imefikisha jumla ya pointi 19 sawa na Yanga inayoongoza kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mchezo ulikuwa mkali na mgumu sana, kila timu ikionekana imedhamiria kushinda lakini Azam ndio iliyokuwa imara zaidi kwa kuzichanga vema karata zake na kupata ushindi huo.
Kama Azam FC ingekuwa makini huenda ingeibuka na ushindi mnono kutokana na kupoteza nafasi nyingi za wazi za kufunga mabao.
Ndanda ilifanya mpira huo kuwa mgumu zaidi kipindi cha pili hasa baada ya kucheza kwa kujihami sana, wakionekana kutafuta sare.
Mara baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall, alisema anashukuru vijana wake wamepata ushindi na kudai kuwa mchezo ulikuwa mgumu sana kutokana na ubovu wa uwanja wa Nangwanda.
"Tumepiga mashuti 12 yaliyolenga lango, hii ni rekodi nzuri inayoonyesha kuwa tuliutawala mchezo kutoka dakika ya kwanza hadi ya mwisho, tulitahidi kupambana licha ya ubovu wa uwanja ni kitu kizuri pia tulicheza kwa nidhamu kubwa mchezoni," alisema.
Naye mfungaji wa bao pekee la Azam FC, Shomari Kapombe, alisema anamshukuru Mungu kwa kuweza kufunga bao lililoipa ushindi Azam.
"Mechi ilikuwa ngumu sana, lakini tuliweza kupambana, tulitengeneza nafasi nyingi, lakini tulizipoteza la muhimu sana tuliweza kuitumia nafasi nzuri tuliyoipata mwishoni mwa mchezo," alisema.
Baada ya ushindi huo, Azam FC inatarajia kuondoka mkoani Mtwara saa 12.30 asubuhi kesho kurejea jijini Dar es Salaam.
Huo unakuwa ushindi wa kwanza wa Azam kwenye Uwanja wa Nangwanda, baada ya msimu uliopita kufungwa bao 1-0 kwenye uwanja huo.
Mpaka sasa Azam FC imecheza mechi tatu za ugenini na kushinda zote ikiwemo hiyo ya Ndanda, awali iliondoka na pointi sita katika Uwanja wa Nangwanda kwa kuzifunga Stand United (2-0) na Mwadui (1-0).
Kikosi cha Azam FC leo kilikuwa hivi: Mwadini Ally, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Aggrey Morris, Pascal Wawa, Said Morad, Frank Domayo, Himid Mao, Ame Ally/Khamis Mcha, Kipre Tchetche/Jean Baptiste Mugiraneza, Ramadhan Singano 'Messi'/John Bocco dk 56
0 Maoni:
Post a Comment