TIMU ya Azam leo jioni imerejea tena kileleni kwa kishindo, baada ya kuichapa Toto Africans mabao 5-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliofanyika Uwanja wa Azam Complex jioni ya leo.
Azam FC imefikisha jumla ya pointi 25 na kuizidi Yanga yenye pointi 23, iliyokaa kileleni kwa saa 24 tokea jana jioni baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 2-0 juzi.
Nyota walioing’arisha Azam FC leo ni beki wa kulia, Shomari Kapombe na mshambuliaji Didier Kavumbagu aliyeanza kuonyesha cheche, kila mmoja akifunga mawili huku Kipre Tchetche akifunga bao jingine.
Timu zote zilianza mchezo huo kwa kupata pigo, dakika ya 16, Toto ililazimika kumtoa kipa Mussa Mohamed baada ya kuumia na kuingia Said Omari, Azam FC nayo ilimtoa Himid Mao aliyechanika kichwani na kuingia Jean Mugiraneza ‘Migi’ dakika ya 29.
Kapombe ndiye aliyeanza kuipa uongozi Azam FC, akifunga bao la kwanza dakika ya 32 kwa kichwa kufuatia krosi safi ya Farid Maliki.
Beki huyo aliyeonekana kucheza vema, aliendelea kutema cheche kwa kuifungia bao la pili dakika mbili baadaye kwa shuti la kiufundi akimalizia pasi ya Kavumbagu, mabao hayo yamemfanya kufikisha bao la tatu msimu huu.
Kipre Tchetche, alifanya kazi nzuri dakika ya 45 kwa kuifungia Azam FC bao la tatu baada ya kugongeana vema mpira na Kavumbagu na yeye kumpa pasi safi ya kisigino kabla ya kumtungua kipa wa Toto Africans, Said Omary, bao hilo limemfanya kutimiza bao lake la sita msimu huu.
Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kuendeleza na moto wao na Kavumbagu aliiandikia bao la nne kwa kwa kichwa dakika ya 47, akimalizia krosi ya Ramadhan Singano ‘Messi’.
Mrundi huyo akaiongezea tena Azam FC bao la tano dakika ya 62 kwa shuti safi baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Toto Africans.
Mabao hayo yamemfanya Kavumbagu kufikisha mabao matatu msimu huu, aliyofunga ndani ya mechi mbili kutoka iliyopita dhidi ya JKT Ruvu waliyoifunga 4-2.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ilipata pigo jingine dakika 52 baada ya kuumia Tchetche na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji wa Kimataifa kutoka Kenya, Allan Wanga.
Katika mchezo huo kulitokea kituko baada ya wachezaji wawili wa Azam FC, kipa Aishi Manula na kiungo Jean Mugiraneza kuugua ghafla homa ya matumbo uwanjani na mpira kulazimika kusimama mara mbili.
Huo ni ushindi wa pili mkubwa mfululizo kwa Azam FC, unaofuatiwa na ule wa kwanza walioupata Alhamisi iliyopita walipoichapa JKT Ruvu 4-2.
Mpaka sasa Azam FC ikiwa kileleni, imefanikiwa kucheza jumla ya mechi tisa ikiwa haijafungwa hata mmoja, ikishinda nane na kutoa sare moja, waliyoipata dhidi ya Yanga (1-1), imefunga jumla ya mabao 20 na kufungwa matano pekee.
Wakati ligi ikisimama kwa takribani mwezi mmoja na wiki mbili, Azam FC itashuka tena dimbani Desemba 12, mwaka huu kukabiliana na Simba, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Vikosi vilikuwa hivi;
Azam FC: Aishi Manula, Shomari Kapombe, David Mwantika, Aggrey Morris, Pascal Wawa, Himid Mao/Jean Mugiraneza (dk 29), Ramadhan Singano ‘Messi’, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche/Allan Wamga (dk52), Farid Maliki/Mudathir Yahya (dk57).
Toto Africans: Mussa Mohamed, Erick Mlilo, Salum Chuku, Hamis Seleman, Hassan Khatib, Abdallah Seseme, Jafet Vedastus, Edward Christopher, Waziri Shemtemba/Madinda Ramadhan (dk60), Evarist Bernard, Miraji Athuman.
0 Maoni:
Post a Comment