Sunday, January 24, 2016

AZAM FC WAPATA MWALIKO ZAMBIA, KUSHIRIKI MICHUANO MAALUMU

Posted By: kj - 7:08 PM

Share

& Comment


KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imealikwa nchini Zambia kushiriki michuano maalumu inayoshirikisha timu nne, iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa klabu mbili za huko, Zesco United na Zanaco FC, itakayoanza kutimua vumbi Jumatano ijayo ndani ya Uwanja wa Levy Mwanawasa jijini Ndola nchini humo.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Azam FC kualikwa kwenye michuano hiyo iliyoanza mwaka 2014, mwaka jana ilishiriki kwa mara ya kwanza ilipofanyika jijini Lubumbashi, Congo DRC na TP Mazembe ikafanikiwa kuibuka mabingwa.

Mwaka huu, Azam FC imealikwa kama mabingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), huku pia ikishirikisha mabingwa wa Ligi Kuu Zimbabwe, Chicken Inn.

Timu nyingine zitakazoshiriki mwaka huu ni mabingwa wa Zambia, Zesco United na Zanaco ya huko, ambao walibeba ubingwa wa Ligi Kuu Zambia mwaka 2012.

Malengo makubwa ya kuanzishwa michuano hiyo ni kuziandaa timu shiriki kuelekea msimu mpya wa ligi zao pamoja na michuano ya Afrika (CAF).

Kwa mujibu wa historia ya michuano hiyo, timu ya Power Dynamos ya Zamzbia ndio timu ya kwanza kutwaa ubingwa huo mwaka juzi kabla ya mwaka jana kuchukuliwa na TP Mazembe, ambayo ilienda kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana.

Timu shiriki za mwaka huu, Azam FC itaiwakilisha Tanzania mwaka huu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika sawa na Zanaco itakayowakilisha kwa upande wa Zambia, huku Chicken Inn ikiiwakilisha Zimbabwe katika Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Zecso United itakayopeperesha bendera ya Zambia katika michuano hiyo.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.