KLABU ya Azam imesema kuwa winga wake Farid Mussa ataendelea kuichezea timu hiyo na hawatamuuza kwa timu yoyote ya nje kama ilivyokuwa ikidaiwa.
Mchezaji huyo ilidaiwa angeihama timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo mwezi huu na alikuwa akihusishwa na kuhamia timu za Celtic FC ya Ligi Kuu ya Scotland au Athletic Bilbao ya Ligi Kuu ya Hispania kwa majaribio.
Akizungumza na gazeti hili jana msemaji wa timu ya Azam FC, Jaffar Iddi alisema kuwa mchezaji huyo ataendelea kuitumikia klabu hiyo kama mkataba wake unavyotaka. Alisema kama klabu haina taarifa rasmi kutokea kwenye timu hizo zilizotajwa kuhusika na kumsajili mchezaji huyo.
Alisema kama klabu katika kuuza mchezaji wake au kumruhusu kwenda kwa majaribio ni lazima utaratibu ufuatwe ambapo alisema kuwa kitu kikubwa ni kuhakikisha kuwa mchezaji anakwenda katika timu husika na sio vinginevyo.
Pia alisema kuwa ni lazima kwa timu yake kujiridhisha na wakala ambaye anaenda kumfuatilia mchezaji husika na ni lazima awe amesajiliwa na kutambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA). Awali, kulikuwa na wakala mmoja mwenye mahusiano mazuri na klabu hizo kuwasiliana na Azam FC akisema Celtic na Bilbao ndizo klabu ambazo zinahitaji mchezaji aina ya Farid.
Chanzo: Habari leo
0 Maoni:
Post a Comment