UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, umesema kuwa bado wataendelea kuutumia uwanja wao wa Azam Complex kwenye mechi za Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu.
Kauli hiyo imekuja siku chache mara baada ya kuripotiwa taarifa mbalimbali zikidai kuwa uwanja huo haujapitishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kama kiwanja cha kuchezea mechi wanazoziandaa kuanzia mwaka huu.
Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz mchana huu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema kuwa uwanja huo una vigezo vyote vinavyotakiwa vya kuchezea mechi za Kimataifa.
“Mashabiki wetu wawe watulivu, mechi zetu zote za Kimataifa tutaendelea kucheza kwenye uwanja wa Azam Complex na si vinginevyo, kwa sababu ndio uwanja wetu wa nyumbani,” alisema.
Alisema kuwa rekodi zipo wazi kabisa kuwa mpaka sasa, tumeshachezea mechi mbili kwa mafanikio, ya kwanza ni ile ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Ferroviario de Beira ya Msumbiji (2014) tuliyoshinda bao 1-0 na nyingine ya Ligi ya Mabingwa Afrika walioifunga mabao 2-0 El Merreikh ya Sudan mwaka jana.
“Kwa mujibu wa TFF, mpaka sasa hakuna mtu wa CAF aliyekuja nchini kukagua viwanja vitakavyochezewa mechi za Kimataifa…hizi taarifa hazipo kwani CAF wenyewe ndio itakayotufahamisha sisi kwa barua kuwa tutachezea wapi mechi zetu, lakini mpaka sasa hatujapokea na bado tunaamini ya kuwa mechi zetu tutachezea nyumbani (Azam Complex),” alisema.
“Hivi uwanja wenye vyumba vya kubadilishia nguo, taa, uzio, ubao wa kusomea matokeo wa elektroniki, chumba cha kupimia wachezaji kubaini wanaotumia dawa za kulevya (doping room), unawezaje kusema hauna vigezo?,” alimaliza kwa kuhoji Kawemba.
Mbali na uwanja huo kutumika kwa mechi za Azam FC, pia zimewahi kufanyika mechi kadhaa za timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ na timu za vijana za wanaume.
Azam FC itaanza kampeni ya kuwania taji la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye raundi ya kwanza kwa kucheza na mshindi wa jumla wa mchezo wa raundi ya awali kati Bidvest Wits ya Afrika Kusini na moja ya klabu kutoka nchini Seychelles.
Kwa mujibu wa droo ya michuano hiyo, inaonyesha kuwa Azam FC itaanza kucheza ugenini dhidi ya mojawapo ya timu hizo kati ya Machi 11, 12 na 13 kabla ya kukipiga nyumbani kati ya Machi 18, 19 na 20.
Azam FC inayoongoza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ikiwa na pointi 35, ikivuka raundi hiyo itatinga raundi ya pili na kukutana na moja ya timu kati ya Esperance ya Tunisia iliyoanzia raundi ya kwanza, ambayo itatakiwa kupita kwa kucheza na mshindi wa mechi ya raundi ya awali kati ya timu kutoka Chad na News Stars de Douala ya Cameroon.
Timu hiyo inayomilikiwa na familia ya Mfanyabiashara maarufu nchini na nje ya mipaka ya Tanzania, Said Salim Bakhresa, itaanzia kucheza nyumbani katika mechi ya raundi ya pili kati ya Aprili 8, 9 na 10 na kumalizia ugenini kati ya Aprili 19 na 20.
0 Maoni:
Post a Comment