KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imejipanga vilivyo kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa kesho wa michuano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Yanga utakaofanyika saa 2.15 usiku katika Uwanja wa Amaan.
Azam FC jana ilianza kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, mchezo wa Kundi B uliokuwa mkali na wa aina yake kwa timu zote kuonyeshana umwamba.
Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kila mchezaji amesikitishwa na kiwango walichokionyesha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar.
“Kila mchezaji amesikitishwa na kiwango, wanajua kuwa hawakucheza vizuri na walifanya makosa, lakini kila mmoja amejipanga kuonyesha mchezo mzuri kesho ili kupata ushindi,” alisema.
Hall alisema anatarajia kukaa na wachezaji tu kujadili kwa kina mchezo wa jana dhidi ya Mtibwa Sugar kujua makosa na kuyasahihisha kabla ya kuvaana na Yanga.
“Mchezo wa kesho utakuwa mgumu, lakini tayari tumejipanga na kila mmoja yupo tayari kwa mechi,” alisema.
“Yanga ina faida kubwa kuelekea mchezo huo kwani sisi tumecheza mechi tatu ngumu ndani ya siku saba, tukianza na Kagera Sugar (Desemba 27) na Mtibwa Sugar (Desemba 30) za Ligi Kuu kabla ya jana kucheza tena huku Yanga ikicheza mechi moja tu ndani ya siku saba, hivyo wamepata muda mrefu wa kupumzika,” alisema.
Aliongeza kuwa sababu hiyo ndio iliyochangia akifanyie marekebisho makubwa kikosi chake jana ili waweze kuwa fiti zaidi katika mchezo wa kesho.
“Hivi sasa Kapombe (Shomari) yupo fiti, Wawa (Pascal) yupo fiti, Racine (Diouf) yupo fiti, Aishi yupo fiti, wote wanaweza kuwa kwenye mchezo wa kesho kwani nitakifanyia marekebisho makubwa kikosi,” alisema.
Katika kujiandaa ipasavyo na mchezo huo, leo asubuhi Azam FC ilifanya mazoezi kwenye Ufukwe wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View, Hall alisema amefanya hivyo ili kuwajenga ufiti wachezaji wake na pia alitumia muda kukiandaa kikosi kitakachocheza kesho na kuwapa mazoezi mepesi wachezaji waliocheza jana.
Ushindi wowote wa Azam FC kwenye mchezo wa kesho utaifanya timu hiyo kutanguliza mguu mmoja mbele kufuzu kwa hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, sare itaifanya kusubiria majaaliwa ya kufika hatua hiyo endapo itaifunga Mafunzo ya Zanzibar katika mchezo wa mwisho.
Mara ya mwisho Azam FC kukutana na Yanga ilikuwa ni kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, walipotoka sare ya bao 1-1, bao la Azam FC likidungwa na Kipre Tchetche huku Donald Ngoma akiwafungia wanajangwani hao.
Benchi la Ufundi la Azam FC lilijiwekea malengo ya muda mrefu ya kuitumia michuano hiyo kuwaangalia wachezaji ambao hawajapata nafasi ya kutosha kucheza mpira kwa kuwapa nafasi ya kucheza kama alivyofanya jana ili kuwaweka fiti.
MSIMAMO KUNDI B
P W D L GF GA P
Yanga 1 1 0 0 3 0 3
Azam FC 1 0 1 0 1 1 1
Mtibwa 1 0 1 0 1 1 1
Mafunzo 1 0 0 0 0 0 0
0 Maoni:
Post a Comment