Wednesday, January 27, 2016

Tunaenda Zambia kujiandaa na Bidvest

Posted By: kj - 11:03 AM

Share

& Comment


KUMEKUWA na malalamiko mengi kutoka kwenye vyombo vya habari, baadhi ya klabu na wadau mbalimbali wa soka nchini mara baada ya Klabu yetu ya Azam FC kupewa ruhusa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kushiriki michuano maalumu nchini Zambia tuliyoalikwa na Zesco United ya huko.

Ikumbukwe ya kuwa Azam FC ni moja ya wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kimataifa mwaka huu, tukishiriki Kombe la Shirikisho Afrika na tutaanza mtihani wetu wa kwanza mwezi Machi kwa kucheza na Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwenye raundi ya kwanza.

tungependa kuweka wazi kuwa, Azam FC imetumia fursa yake ambayo kwenye ratiba ya VPL inaonesha kuwa ilikuwa na ruhusa ya kutocheza baadhi ya mechi ili kupisha mashindano ya shirikisho la Afrika ambayo Azam FC ni wawakilishi. Mechi za raundi ya 19 na 22 dhidi ya Coastal Union na Mtibwa Sugar zingeahirishwa. kwa hiyo safari hii nchini Zambia, timu itakosa mechi zetu mbili tu za ligi ilizotakiwa kucheza na Tanzania Prisons na Stand United.  

Klabu ya Azam FC inapenda kutoa shukrani za dhati kwa uongozi wa TFF kwa kutambua umuhimu wa kujiandaa kisayansi na kuweza kutupa ruhusa hiyo maalumu, kwani wametambua ya kuwa Azam FC inahitaji fursa ya kujiandaa vema ili kuweza kupeperusha vema bendera ya Tanzania katika michuano hiyo ya kimataifa, tena ikizingatiwa timu tunayokutana nayo Bidvest Wits itakuwa na maandalizi ya kutosha kwa kuwa imeanzia raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam FC tukiwa nchini Zambia tunatarajia kucheza na wenyeji wetu Zesco United na Zanaco FC zote kutoka Zambia pamoja na mabingwa wa Zimbabwe, Chicken Inn, timu zote zikitokea kusini mwa Afrika, ukanda ambao wanatokea Bidvest Wits, hivyo tunaamini ya kuwa kupitia michuano hiyo tutakuwa tumepata maandalizi ya kutosha kabla ya kuvaana na Bidvest Wits.

Mara kwa mara klabu za Tanzania zimekuwa zikipata malalamiko mbalimbali kutoka kwa wadau mbalimbali pale zinaposhindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa na sababu kubwa inayokuwa ikitolewa ni timu kukosa maandalizi ya kutosha. Bahati mbaya watoa lawama timu zinapofanya vibaya leo wamegeuka na kutoa lawama kwa uongozi wa Azam FC na TFF tunapojaribu kufuta sababu zinazopelekea timu kufanya vibaya.

Sababu mojawapo ni uchache au kukosa mechi za majaribio za kimataifa, hivyo uongozi wa Azam FC umekuwa ukifanya jitihada za hali na mali kuhakikisha unaipa timu maandalizi ya kisayansi ili kuepusha sababu toka kwa benchi la ufundi endapo timu itashindwa kufanya vema katika michuano ya kimataifa.

Maandalizi hayo yamekuwa yakiigharimu Azam FC fedha nyingi, lakini kwa mapenzi yake kwa nchi na katika kuhakikisha klabu za Tanzania tunapiga hatua katika mashindano ya kimataifa, hivyo uongozi wa Azam FC umekuwa haujali gharama hizo hasa kama zitasaidia kufanya vema katika michuano hiyo.

Tunaomba wadau waelewe kuwa safari hii ya Azam FC si ya kujifurahisha bali ni safari muhimu ya kujiandaa kwa lengo la kuiwakilisha vema nchi kwani malengo ya Azam FC ni kubadili hali iliyokuwepo huko nyuma na kuona vilabu vya Tanzania vikifika robo fainali au hata kutwaa ubingwa wa Afrika.

Imetolewa na Idara ya Ufundi ya Azam FC

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.