Azam FC KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuweka kambi nje ya nchi kujiandaa na mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini.
Azam FC ina nafasi kubwa ya kukutana na Bidvest, ambayo imetoka kushinda mabao 3-0 dhidi ya Light Stars ya Shelisheli kwenye mchezo wa raundi ya awali ya michuano hiyo na sasa watacheza mchezo wa marudiano, jijini Johannesburg, Afrika Kusini wikiendi hii.
Mchezo wa kwanza baina ya Azam FC na Bidvest Wits unatarajia kufanyika Machi 12 mwaka huu kwenye Uwanja wa Bidvest jijini Johannesburg saa 12.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki kabla ya kurudiana nao Azam Complex Machi 20 mwaka huu saa 9.00 Alasiri.
Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema kuwa kambi hiyo maalumu wataiweka kwenye nchi jirani na Afrika Kusini kwa siku nne kabla ya kuelekea jijini Johannesburg siku moja kabla ya mchezo huo.
“Tunamshukuru mwenyezi Mungu, tulipata nafasi ya kwenda jijini Ndola (Zambia), ile ilikuwa ni sehemu yetu ya kujiandaa na mechi za Kimataifa, watu walitubeza lakini tunasema ndio hivyo na kwa maana ya kuelekea kwenye mechi hiyo Kocha kashaweka programu yake na tayari utawala umeshaifanyia kazi programu hiyo.
“Kwamba timu itaweka kambi nje ya nchi kwa takribani siku nne katika moja ya nchi jirani na Afrika Kusini tutakaa hapo na baadaye tutakwenda Johannesburg moja kwa moja siku moja kabla ya mechi,” alisema.
Kawemba alisema mara baada ya mchezo huo watarajea kwenye nchi waliyoweka kambi kuendelea na maandalizi na watatua jijini Dar es Salaam siku moja kabla ya mchezo wao wa kiporo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Stand United utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Machi 16, mwaka huu.
”Baada ya mchezo wetu dhidi ya Stand United, tutarejeana na Bidvest na tumekuwa kwenye mawasiliano nao na tumeshajua kuwa mchezo wetu wa kwanza dhidi yao utakuwa Jumamosi jioni Machi 12, hivyo washabiki wetu wasiwe na wasiwasi,” alisema.
Katika kambi yake ya kwanza ya mandalizi jijini Ndola Zambia, Azam FC iliweza kutwaa ubingwa maalumu nchini humo mbele ya timu wenyeji za Zesco United na Zanaco FC pamoja na mabingwa wa Zimbabwe, Chicken Inn.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB imejiwekea malengo ya kufika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mwaka huu, ikivuka raundi hiyo kwenye raundi ya pili itakutana na moja ya timu tatu kati ya Esperance de Tunis ya Tunisia inayoanzia sawa nao raundi ya kwanza au Renaissance FC ya Chad na New Star de Douala ya Cameroon, ambazo zinachuana raundi ya awali. Esperance inasubiria kucheza na moja ya timu hizo kati ya Renaissance na New Star de Douala katika raundi ya kwanza kabla ya kukutana Azam FC au Bidvest Wits kwenye raundi ya pili itakayoanza mwezi Aprili mwaka huu.
0 Maoni:
Post a Comment