Tuesday, February 9, 2016

Hall: Tutaendeleza rekodi yetu ugenini vs Coastal Union

Posted By: dada - 7:33 PM

Share

& Comment

KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa wameweka malengo ya kushinda mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ili kuendeleza rekodi yao nzuri ya mechi za ugenini.

Azam FC mpaka sasa imecheza mechi saba ugenini, ikishinda sita na kutoa sare mchezo mmoja dhidi ya Yanga (1-1) katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kitakwimu imekusanya pointi 19 ugenini kati ya 21 ilizotakiwa kuzipata.

Coastal Union iliyojikusanyia jumla ya 13 katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi, ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, mabao yaliyofungwa na Shomari Kapombe na Kipre Tchetche.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Hall alisema anajua mchezo huo utakuwa mgumu lakini wamejipanga kushinda, huku akisisitiza kuwa wana rekodi nzuri ya ushindi katika Uwanja wa Mkwakwani, mjini Tanga wanakoenda kuchezea.

“Baada ya mchezo wa Jumapili iliyopita dhidi ya Mwadui wachezaji wangu wameonekana kuchoka hasa kutokana na ziara ya Zambia, hivyo najaribu kurudisha nishati kwa wachezaji wangu na kurejesha furaha ya kila mmoja kwa kuwapa mazoezi sahihi leo na kesho, kwa sababu unapokuwa umechoka ni ngumu kuwa na furaha kwa kuwa unajijua ya kuwa umechoka, hivyo nitaanza kuwapa mbinu za mchezo huo Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi,” alisema.

Hall aliongeza kuwa: “Tutasafiri kwenda Tanga Ijumaa na tutafanya mazoezi yetu kwenye uwanja tutakaochezea Jumamosi, tunaijua Tanga tumeanza kwenda pale miaka mingi, tunajua kuwa kuna hali ngumu, kila mmoja amepata wakati mgumu Tanga, tunajua kuwa Yanga, Simba wamepata shida pale, lakini kwetu sisi tumekuwa na rekodi nzuri pale na tunatakiwa kuiendeleza kwa kushinda mchezo.”

Akizungumzia michezo miwili ya kiporo waliyokuwa nayo dhidi ya Tanzania Prisons (Februari 24) na Stand United (Machi 16), Hall alisema wana nafasi kubwa ya kukaa kwenye nafasi bora katika msimamo wa ligi kama watashinda mechi hizo.

“Jambo zuri hivi sasa kila mtu na magazeti yote ni wamekuwa wakizimulika Simba, Yanga, kwa sababu ukiangalia kwenye msimamo unaonyesha kuwa Yanga, Simba na Azam FC ikifuatia, hivyo sisi hivi sasa tupo kimya ambalo ni jambo zuri kwetu, tunawaache wapinzani wetu waongee, magazeti yatabiri bingwa kama ni Simba au Yanga, na kila mmoja ametusahau sisi kitu ambacho ni kizuri,” alisema.

Aidha alisema kuwa ameshaweka wazi kuwa bingwa wa ligi hawezi kupatikana kwa timu kuongoza ligi mwezi Januari na Februari, bali timu inatayotwaa ubingwa ni ile iliyokaa kileleni kuanzia mwezi Aprili na Mei, ligi inapoelekea kumalizika.

Ukiondoa rekodi nzuri ya mechi za ugenini, Azam FC mpaka sasa pia imeshacheza michezo tisa nyumbani ikishinda saba na kutoa sare mechi mbili, mmoja ukiwa ni ule waliochezana Simba katika Uwanja wa Taifa (2-2) huku sare nyingine wakitoa na African Sports (1-1) katika Uwanja wa Azam Complex.

Hivyo kitakwimu mpaka sasa kwenye mechi hizo walizocheza nyumbani, Azam FC imezoa pointi 23 kati ya 27 walizotakiwa kuzipata.

Jambo zuri zaidi miongoni mwa timu 16 za ligi, Azam FC ndio timu pekee ambayo haijafungwa mchezo wowote, ikishinda 13 na sare tatu na kujikita katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikifikisha pointi 42 sawa na Simba iliyo nafasi ya pili na Yanga iliyo kileleni kwa pointi 43, lakini matajiri hao wa Azam Complex wanamichezo miwili mkononi.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.