Sunday, February 14, 2016

Rekodi ya Azam FC yatibuliwa Mkwakwani

Posted By: dada - 9:00 PM

Share

& Comment

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo imepoteza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu baada ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, mchezo uliofanyika jioni hii kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Azam FC kufungwa mchezo huo kunaifanya ipoteze rekodi yake ya kutofungwa mchezo wowote wa ligi kwa siku 286 (mechi 18), ambapo hadi inafungwa leo na Coastal ilikuwa haijapoteza mchezo wowote wa ligi tokea ilipofungwa mara ya mwisho na Simba (2-1) Mei 2, mwaka jana.

Vilevile huu ndio mchezo wa kwanza kwa Azam FC kupoteza ugenini msimu huu ndani ya mechi nane walizocheza, ikiwa imeshinda sita, sare moja dhidi ya Yanga (1-1) na kupoteza huo mmoja.

Kikosi cha Azam FC leo kilijitupa uwanjani bila uwepo wa mabeki wake wanne wa kati, Abdallah Kheri, David Mwantika, Aggrey Morris na Racine Diouf  huku washambuliaji Didier Kavumbagu na Ame Ally, nao wakiwa majeruhi.

Bao pekee la Coastal Union leo limefungwa dakika ya 68 na beki Miraj Adam kwa mpira wa moja kwa moja wa adhabu ndogo ya ndani ya eneo la 18 (indirect free kick).

Mwamuzi aliamuru upigwe mpira huo akidai kuwa kipa wa Azam FC, Aishi Manula, hakuutoa mpira nje kuashiria kuomba mpira usimame baada ya kuumia wakati alipokuwa kwenye harakati za kudaka mpira.

Azam FC ingeweza kujipatia mabao mawili kama mshambuliaji wake Allan Wanga, angekuwa makini kutumia nafasi mbili alizozipata kipindi cha kwanza baada ya moja kupaisha juu mpira akiwa ndani ya eneo la 18 katika dakika 11.

Huo ni ushindi wa kwanza kwa Coastal Union dhidi ya Azam FC kwenye mechi za ligi, ambapo katika mechi 10 walizokutana, matajiri hao wa Azam Complex wameshinda mechi saba, sare mbili na huo mmoja wakipoteza leo.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC ibakie katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 42 ikizidiwa pointi tatu na kinara Simba anayeongoza. lakini wekundu hao wamecheza mechi mbili zaidi ya matajiri hao huku Yanga inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 43 nayo ikiizidi Azam FC mchezo mmoja.

Azam FC itashuka dimbani tena Jumamosi ijayo kuvaana na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya kabla ya Februari 24 kucheza mechi ya kwanza ya kiporo dhidi ya Tanzania Prisons kwenye uwanja huo huo.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Farid Mussa/Gadiel Michael dk 45, Shomari Kapombe, Pascal Wawa, Said Morad, Erasto Nyoni, Jean Mugiraneza, Frank Domayo/Salum Abubakar dk 45, Michael Bolou, John Bocco (C), Allan Wanga/Kipre Tchetche dk 69

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.