Thursday, March 31, 2016

KAPOMBE AINYANYUA AZAM FC, WAKISHINDA GOLI 3 NA KUTINGA NUSU

Posted By: kj - 6:08 PM

Share

& Comment


KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imetinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuitoa nishai Tanzania Prisons kwa kuichapa mabao 3-1 jioni ya leo ndani ya Uwanja wa Azam Complex.

Huo ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Azam FC kwenye michuano hiyo baada ya awali kuipiga African Lyon (4-0) na ikaitupa nje Panone ya mjini Moshi kwa kuinyuka mabao 2-1 katika mchezo wa hatua ya 16 bora.

Azam FC ilianza kuonyesha toka mwanzo kuwa imepania kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuanza mchezo huo kwa kasi na kulishambulia mfulizo lango la maafande hao.

Shujaa wa mabingwa hao wa Kombe la Kagame, alikuwa ni beki Shomari Kapombe, aliyeendeleza wimbi lake la kufunga mabao baada ya kuipatia bao la uongozi dakika ya tisa tu kwa shuti zuri la kifundi nje ya eneo la 18 lililomshinda kipa wa Prisons, Beno Kakolanya kufuatia pasi safi ya Didier Kavumbagu.

Prisons waliamka baada ya dakika 25 za kwanza na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 31 lililofungwa na mshambuliaji Jeremiah Juma, aliyetumia uzembe wa mabeki wa Azam FC.

Licha ya Azam FC kuendelea kutafuta bao la pili, jitihada hizo ziligonga mwamba hadi kipindi cha kwanza kinamalizika kutokana na washambuliaji walioanza John Bocco ‘Adebayor’ na Didier Kavumbagu kubanwa na mabeki wa Prisons.

Mabadiliko yaliyofanywa na benchi la ufundi la Azam FC kipindi cha pili ya kumtoa beki Wazir Salum na kuingia Frank Domayo, yaliweza kubadilisha taswira ya mchezo huo baada ya matajiri hao kumiliki eneo la kiungo jambo ambalo liliwafanya Prisons kupanga mashambulizi kupitia pembeni mwa uwanja.

Juhudi za Azam FC kusaka bao la pili zilizaa matunda dakika ya 50 baada ya Kapombe kufunga bao lake la pili kwenye mchezo huo kwa shuti kali baada ya kugongeana vema Sure Boy, aliyeendeleza kiwango chake kizuri dimbani leo.

Hilo ni bao la11 kwa Kapombe msimu huu, akiwa amewafunika mabeki wenzake na baadhi ya washambuliaji Tanzania, nane akifunga Ligi Kuu na moja katika Kombe la Shirikisho Afrika na mawili akitupia FA Cup.

Mcha aliihakikishia Azam FC nafasi ya kwenda nusu fainali baada ya kupiga bao la tatu dakika ya 86 baada ya kumuhadaa beki mmoja wa Prisons na kupiga shuti zuri lililojaa kimiani, hilo ni bao la kwanza kwa winga huyo msimu huu ambaye ameanza kucheza baada ya kutoka kuuguza majeraha ya goti yaliyomtesa msimu uliopita.

Wachezaji wa Azam FC waliendelea na kasi ya kusaka bao jingine, ambapo almanusura kiungo Michael Bolou aifunge bao la nne kufuatia shuti kali alilopiga nje kidogo ya eneo la 18 na mpira kugonga mwamba wa juu na kutoka nje na hivyo hadi dakika 90 zimalizika timu hiyo iliondoka kifua mbele.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alilazimika kuwachezesha Kapombe na Bocco waliokuwa wana homa ya mafua kutokana na umuhimu wa mchezo huo.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki bora kabisa nchini ya NMB, imeungana na timu nyingine za Mwadui na Yanga kutinga hatua ya nusu fainali huku wakiisubiria timu nyingine ya nne kati ya Simba na Coastal Union, ambazo zitachuana Aprili 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Shomari Kapombe/Farid Mussa (dk 80), Wazir Salum/Frank Domayo (dk 46), Aggrey Morris, Serge Wawa, Erasto Nyoni, Michael Bolou, Salum Abubakar, Ramadhani Singano, John Bocco/Khamis Mcha (dk 60) na Didier Kavumbagu.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.