Monday, March 7, 2016

Marinica: Waamuzi wametunyima ushindi v Yanga

Posted By: dada - 8:00 PM

Share

& Comment


KOCHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Mario Marinica, amesema kuwa waamuzi wa mchezo wao dhidi ya Yanga juzi ndio wamewanyima ushindi baada ya kukataa bao halali lililofungwa na beki wa kulia Shomari Kapombe.

Kapombe alifunga bao hilo dakika ya 20 kwa kichwa akiunganisha krosi iliyopigwa na winga Farid Mussa, lakini cha kushangaza mwamuzi msaidizi namba moja, Soud Lilla, alidai mfungaji alikuwa ameotea maamuzi ambayo hayakuwa na uhalali.

Baada ya dakika 90 kumalizika ilishuhudiwa timu hizo zikienda sare ya mabao 2-2 na kuendeleza rekodi yao ya upinzani mkali, kwani mpaka sasa kwenye mechi 16 za ligi walizokutana, kila upande umeshinda mara tano na kutoa sare mara sita tokea msimu wa 2008/2009, Azam FC ilipoanza kucheza Ligi Kuu.

“Ilikuwa ni mechi ya kuburudisha, ngumu tulipambana vizuri kwenye mchezo huo hadi kutoka nyuma ya mabao 2-1 na kusawazisha, na tulipambana na kila mmoja, tulicheza mpira mzuri na kufunga mabao matatu, lakini waamuzi walilikataa bao letu moja alilofunga Kapombe (Shomari).

“Yanga imeshindwa kutufunga kwenye mechi ya tano sasa msimu huu, licha ya waamuzi kuwa upande wao kila tunapocheza nao na TFF ikitaka washinde, lakini hayo yote yameshindikana kwa kuwa sisi ni timu bora,” alisema Marinica wakati akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz.

Akizungumzia mbio zao za ubingwa wa ligi hiyo, Marinica alisema bado wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na Azam FC kuwa ni timu bora kuliko nyingine hapa nchini.

“Hilo liko wazi tunaweza kutwaa ubingwa kwa kuwa sisi ni timu bora, hakuna timu iliyoweza kutufunga, ni Coastal Union tu ndio imeweza kutufunga baada ya baadhi ya makosa tuliyofanya, lakini zaidi hiyo hakuna timu iliyoweza kufanya hivyo,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, hivi sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 47 sawa na Yanga iliyo nafasi ya pili, lakini timu hizo zina mchezo mmoja mkononi dhidi ya Simba ambayo ipo kileleni kwa pointi 48.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.