Wednesday, March 2, 2016

WANGA: NITAENDELEA KUFUNGA

Posted By: kj - 6:18 PM

Share

& Comment


BAADA ya kuifungia Azam FC bao la ushindi dhidi ya Panone, mshambuliaji Allan Wanga anachofikiria zaidi hivi sasa ni kufunga mabao zaidi kufuatia kuondoa ukame wa mabao uliokuwa umemuathiri kiakili.

Kauli hiyo ya Wanga imekuja baada ya juzi kuiwezesha Azam FC kushinda mabao 2-1 dhidi ya Panone kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, ukiwa ni mchezo wa raundi ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz Wanga alisema alikuwa akilisubiria kwa muda mrefu bao hilo na amelipokea kwa furaha kubwa hasa baada ya kuiwezesha Azam FC kupata ushindi huo.

“Nafuraha kufunga kwani sijafanya hivi muda mrefu, nilikuwa na matatizo mengi labda yakaniathiri kiakili, lakini namshukuru Mungu, nashukuru wachezaji wenzangu, nashukuru benchi la ufundi na viongozi wote pamoja na mashabiki kwa sapoti wanayonipa, nimeweza kufunga bao nililokuwa nasubiria kwa muda mrefu.

“Ujue mshambuliaji ukikaa muda mrefu bila kufunga pia inakuathiri, baada ya kufunga bao hilo la kwanza ni furaha tu niliyonayo, nitaendelea kufanya bidii na kufunga zaidi kwani bao hilo litaniongezea morali zaidi ya kufunga mengine,” alisema.


Anazungumziaje uwanja?


Wanga hakusita kuelezea hali mbaya ya Uwanja wa Ushirika waliochezea mechi hiyo na kudai kuwa iliwapa wakati mgumu wao kama wachezaji katika kusaka ushindi huo.

“Ni mara yangu ya kwanza kucheza kwenye kiwanja kama hiki kwa sababu kimetupatia wakati mgumu sana, mara nyingi tumekuwa tukifanya mazoezi pale Chamazi (Azam Complex) na hata mechi nyingi tulizochezea kwenye uwanja mbovu havifikii hiki kwa ubovu.

“Imetusumbua sana kipindi cha kwanza na mwanzoni mwa kipindi cha pili kwa sababu hata ukipewa pasi unafikiria kwanza kiwanja, namna ya kuupokea mpir a na sehemu utakapotulia, huku pia ukiwa unakabiliana na  adui nyuma yako, lakini nashukuru tumepata ushindi,” alimalizia Wanga.

Hilo linakuwa bao la pili kwa Wanga ndani ya Azam FC tokea ajiunge na timu hiyo Julai mwaka jana, bao la kwanza alifunga wakati walipoifunga Stand United mabao 2-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga Septemba mwaka jana.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.