Tuesday, April 19, 2016

MATCH PREVIEW: AZAM Vs ESPERANCE

Posted By: dada - 6:20 AM

Share

& Comment

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo saa 3.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki itakuwa na shughuli pevu pale itakapokuwa ikikabiliana na wenyeji wao Esperance de Tunis katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Mchezo huo wa raundi ya pili ya michuano hiyo utafanyika katika Uwanja wa Olympique de Rades na Azam FC inahitaji ushindi wowote au sare yoyote ili kusonga mbele kutokana na ushindi wa mabao 2-1 walioupata jijini Dar es Salaam wiki moja iliyopita.

Mabao ya Azam FC katika mchezo huo yaliwekwa kimiani na mawinga machachari Ramadhan Singano ‘Messi’ na Farid Mussa, waliofanikiwa kuonyesha kiwango kizuri na kuleta madhara makubwa kwenye safu ya ulinzi ya Esperance.

Wachezaji wa Azam FC wana morali kubwa kuelekea mchezo huo, hata katika mazoezi ya juzi na jana wameonekana kufanya kwa ari kubwa na bidii jambo ambalo linaonyesha kila dalili kwa timu hiyo kupata matokeo mazuri kesho.

Kauli ya benchi la ufundi


Akizungumzia namna walivyojipanga kwa mchezo huo baada ya mazoezi ya jana usiku, Kocha Mkuu wa Azam FC Stewart Hall, amesema kuwa wachezaji wana hali nzuri kuelekea mechi hiyo huku akiamini ya kuwa watapata matokeo mazuri.

“Uwanja ni mzuri sana, wachezaji nao walivyouona kwa mara ya kwanza wameukubali mno, sehemu ya kuchezea ni nzuri kwa ajili ya mpira kuchezwa, inaruhusu mpira kuchezeka haraka, mpira utakuwa ni haraka sana kutokana na nyasi za uwanja kuwa fupi, hivyo kutakuwa na mpira mzuri sana kesho (leo),” alisema.

Hall alisema kuwa wanatarajia kufanya kazi nzuri licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji wake wanaosumbuliwa na majeraha akiwemo beki Shomari Kapombe ambaye ni mgonjwa.

“Tunatakiwa kukabiliana na hali hiyo kwa kufanya kazi yetu kwa bidii uwanjani, pia lazima tujipange vizuri ili kupata matokeo tunayoyataka, najua kikosi changu kitaathirika kwa kuwakosa wachezaji hao, lakini tupo tayari kwa mapambano,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ na Sofapaka ya Kenya, aliongeza kuwa: “Jambo kubwa tunalotakiwa kuhakikisha kesho (leo) ni kuwa vizuri katika eneo la ulinzi na iliyopangika vizuri, baada ya hiyo hapo ndipo utapata msingi mzuri kuelekea maeneo mengine uwanjani, unajua unapojenga nyumba huwezi kuanza kuweka paa kwanza lazima uanze na msingi, ambapo jambo kubwa la kukuwezesha kushinda kwenye mpira ni kujenga vema eneo la ulinzi.”

Wachezaji nao walonga


Nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, amesema wamemaliza vema maandalizi ya mchezo huo huku akidai kuwa kila mchezaji ana morali kubwa kuelekea mchezo huo.

“Mazoezi ya mwisho leo (jana) yalikuwa mazuri tumemaliza salama, yalikuwa na morali kubwa kilichobaki ni wachezaji kwenda kujituma tu uwanjani kesho (leo) na Mungu atatusaidia sisi kupambana na kuweza kupata matokeo mazuri, lakini tunaiheshimu Esperance kuwa ni timu kubwa,” alisema.

Naye mshambuliaji nyota kutoka Burundi Didier Kavumbagu, alisema kuwa wamejipanga kuweza kukabiliana na yote watakayokutana nayo uwanjani leo na kuweza kupata matokeo wanayoyahitaji.

“Azam FC mpaka sasa ninapozungumza tunanafasi kubwa ya kusonga mbele, lakini yote itatokana na namna tutakavyocheza mchezo wa kesho (leo), lakini ni lazima wachezaji tujitume kwa moyo wetu wote na kuwa kitu kimoja uwanjani na kupigana kwa namna tulivyopigana katika mchezo wa kwanza pamoja na kuzidisha bidii zaidi ili tuweze kufuzu,” alisema.

Kwa upande wake mfungaji wa bao la ushindi kwenye mchezo wa Dar es Salaam, Ramadhan Singano ‘Messi’, alisema kuwa wanaamini ya kuwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kesho (leo) watapata matokeo yale ambayo timu inayategemea pamoja na Watanzania kwa ujumla.

“Mimi kwa timu yoyote ambayo tunakutana nayo huwa najiandaa vizuri, na hata huo wa kesho (leo) nao nitajiandaa vizuri ili kuwapa faida timu yangu ya Azam, Mwenyezi Mungu anajua sisi tunanafasi gani katika mchezo huo, ila naamini tutafanya vizuri,” alisema Singano.

Rekodi mpaka sasa


Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, imefanikiwa kufunga mabao tisa na kufungwa manne mpaka sasa katika mechi tatu za michuano hiyo walizocheza mpaka sasa, saba wakifunga ilipocheza na Bidvest Wits ya Afrika Kusini na kuitoa kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-3 na mawili walipoichapa Esperance 2-1 jijini Dar es Salaam.

Katika mechi zote hizo tatu, Azam FC haijafungwa mchezo wowote ikiwa na ushindi wa asilimia 100 na anayeongoza kuifungia mabao ni Kipre Tchetche, aliyefunga matatu mpaka sasa na nahodha Bocco akifunga mawili ndani ya michuano hiyo.

Nidhamu juu Azam FC

Hadi Azam FC inacheza mchezo wa nne leo wa michuano hiyo, hadi sasa ni miongoni mwa timu zenye nidhamu kubwa ya mchezo kutokana na kukusanya kadi mbili tu za njano huku ikiwa haina kadi yoyote nyekundu.

Kadi hizo zote za njano amezipata kiungo mkabaji raia wa Rwanda, Jean Baptiste Mugiraneza, ambaye ataukosa mchezo huo kwa kukusanya idadi hizo za kadi, lakini wapinzani wao Esperance mpaka sasa wamekusanya kadi nane za njano.


Namna ya kupata matokeo

Ili kuweza kupata kila kinachojiri katika mchezo huo, tunakuomba ewe shabiki wa Azam FC na Watanzania kwa ujumla mtembelee ukurasa rasmi wa klabu wa mtandao wa kijamii wa facebook kwa kuandika na kulike ‘Azam FC’.

Kama hiyo haitoshi uongozi wa Azam FC unavyowajali mashabiki wa timu hiyo na Watanzania kwa ujumla kwa sasa iko kwenye hatua za mwisho kuweza kukuletea mechi hiyo ‘live’ kupitia kingamuzi bora kabisa cha Azam TV, hivyo mpaka sasa kuna uhakika wa asilimia 10 mchezo huo kuonyeshwa.

Hatua ijayo itakavyokuwa

Azam FC ikifanikiwa kusonga mbele itafuzu kwa hatua ya mwisho ya mtoano (play off), huko itapangiwa moja ya timu nane zilizotolewa kwenye raundi ya mwisho ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikipenya hapo tena itaenda moja kwa moja katika hatua ya makundi (robo fainali).

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.