Azam FC tayari imewasili nchini Tunisia tokea jana kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano utakaofanyika kesho Jumanne saa 3.00 kwa saa za Afrika Mashariki, wameingia wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-1 walioupata awali jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Migi alisema Azam FC ina wachezaji wengi wazoefu na wazuri jambo ambalo linampa matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo huo.
“Nawajua Esperance, nimecheza nao mara nne nilipokuwa nacheza APR, mara zote nyumbani kwetu tulikuwa tunatoa nao sare au kushinda bao moja, lakini wamekuwa wakitufunga kwao, wanapocheza nyumbani wanapenda sana kumiliki mpira kwa kucheza pasi na pia waamuzi mara nyingi walikuwa upande wao kuwapendelea,” alisema.
Migi alisema wanatakiwa kuwa makini sana katika mchezo huo kwa kukabiliana na presha kutoka kwa wapinzani wao ili waweze kupata matokeo wanayohitaji.
Kiungo huyo kutoka Rwanda tokea ajiunge na Azam FC Julai mwaka jana, amekuwa nguzo muhimu kwa timu hiyo kwenye eneo la kiungo wa ukabaji, akiwa na uwezo wa kucheza mipira ya juu na ya chini pamoja na kutibua mashambulizi ya timu pinzani.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB inahitaji sare yoyote au ushindi ili iweze kusonga mbele kwa hatua ya 16 bora (play off), itakapokutana na moja ya timu iliyotoka kwenye hatua hiyo ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikifuzu hapo itatinga moja kwa moja katika hatua ya makundi ya michuano hiyo (robo fainali).
0 Maoni:
Post a Comment