Mchezo huo ni muhimu kwa Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB katika kuendeleza mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo walioupoteza msimu uliopita baada ya kuchukuliwa na Yanga.
Tchetche aliyeanza kufanya mazoezi na timu tokea timu hiyo ikijiandaa na mechi dhidi ya Majimaji, alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya enka aliyopata kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar uliofanyika Uwanja wa Manungu, Morogoro ambao Azam FC ilishinda bao 1-0 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na nahodha John Bocco ‘Adebayor’.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Stewart Hall, ameuthibitishia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz leo kuwa Tchetche yupo fiti kwa ajili ya mchezo huo baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakimkabili.
Katika hatua nyingine kiungo Frank Domayo, aliyepata maumivu ya enka wakati wa mchezo wa Mwadui, yeye atakuwa fiti baada ya wiki mbili zijazo na sasa anaendelea na matibabu chini ya jopo la madaktari wa Azam FC.
Kuhusu uwepo wa wachezaji wengine kama vile Pascal Wawa, Allan Wanga, Wazir Salum, Racine Diouf itajulikana mara baada ya mazoezi ya mwisho ya Azam FC kesho kabla ya kuwavaa Wekundu hao wa Msimbazi.
Kiungo Himid Mao 'Ninja' yeye ataendelea kukosekana kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata kwenye mchezo namba 170 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Azam FC iliyobakisha michezo mitano ya ligi, mpaka sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa imejikusanyia pointi 58, Simba yenyewe imejizolea pointi 57 katika nafasi ya tatu huku Yanga ikiwa kileleni baada ya kufikisha pointi 62.
0 Maoni:
Post a Comment