Thursday, May 5, 2016

JKT RUVU AZAM FC WATOKA SARE

Posted By: kj - 12:13 PM

Share

& Comment

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jana jioni imelazimishwa sare ya mabao 2-2 na JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Sare hiyo imeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 60 katika nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 27 na itaweza kumaliza ligi ikiwa na pointi 69 endapo itashinda mechi zake tatu zilizobakia, huku Simba yenye mchezo mmoja mkononi ikiwa nazo 58 na itamaliza katika nafasi ya pili kama itashinda michezo minne waliyobakisha (70).

Matokeo hayo yamefifisha mbio za Azam FC za kuwania ubingwa wa ligi kwani vinara Yanga wanahitaji ushindi wowote Mei 10, mwaka huu watakapocheza na Mbeya City katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya ili wafikishe pointi 71 ambazo hazitaweza kufikiwa na timu nyingine ya ligi hiyo.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, itabidi ijilaumu yenyewe katika mchezo huo kwani iliweza kumaliza kipindi cha kwanza ikiwa mbele kwa mabao 2-0 huku ikipoteza nafasi nyingi za wazi za kufunga mabao kupitia kwa washambuliaji wake Kipre Tchetche na nahodha John Bocco ‘Adebayor’.

Mabao ya wenyeji hao yaliwekwa wavuni na mapacha Michael Bolou aliyefunga bao la kwanza dakika ya 31 na Kipre Tchetche dakika ya 37, wote wakipokea pasi safi kutoka kwa Himid Mao ‘Ninja’, ambaye kipindi hicho alicheza kama winga wa kulia.

Kipindi cha pili Azam FC ililazimika kufanya mabadiliko ya kuingia beki Said Morad na kutoka David Mwantika, ambaye alikuwa akijisikia vibaya kufuatia kugongana na mchezaji mmoja wa JKT Ruvu.

JKT Ruvu inayonolewa na kocha mkongwe Abdallah Kibadeni ‘King’, ilirejea mchezoni kipindi cha pili kufuatia kasi ya wachezaji wa Azam FC kupungua hali iliyowafanya kusawazisha mabao yote mawili na kuambulia sare hiyo.

Alikuwa ni Saady Kipanga aliyeipatia bao la kwanza JKT Ruvu dakika ya 56 kwa njia ya mkwaju wa penalti kufuatia Gadiel Michael kuunawa mpira ndani ya eneo la 18 na mwamuzi Seleman Kinungai kutoka Morogoro akaashiria ipigwe adhabu hiyo ndogo kuelekea lango la Azam FC.

JKT Ruvu iliendelea kuongeza kasi na hatimaye ikapata bao la kusawazisha lililofungwa na Najim Magulu baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Azam FC, na hadi dakika 90 zinamalizika timu hizo ziliambulia sare hiyo na kugawana pointi moja kila mmoja.

Hiyo ni sare ya pili mfululizo kwa Azam FC baada ya wikiendi iliyopita kutoka suluhu na Simba ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa inataka kubakia katika nafasi yake ya pili mabingwa hao wanahitaji kushinda mechi zote tatu zilizobakia na kuwaombea wekundu hao wateleze mchezo mmoja kati ya minne waliyobakiwa nayo.

Kikosi cha Azam FC kinatarajia kushuka tena dimbani Jumapili hii Mei 8 katika Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga kuvaana na wenyeji wao Kagera Sugar, ambayo ipo kwenye vita ya kupigania kutoshuka daraja.


Vikosi vilivyocheza:

Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Abdallah Kheri, David Mwantika/Said Morad dk46, Himid Mao, Kipre Balou/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk80, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk64, John Bocco na Kipre Tchetche.

JKT Ruvu; Madenge Ramadhani, Hamisi Seif, Omar Kindamba, Paul Mhidze, Renatus Morris, Nashon Naftali, Abdulrahman Mussa/Samuel Kamuntu dk46, Hassan Dilunga, Najim Magulu, Mussa Juma na Saad Kipanga/George Minja dk 89.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.