MSHAMBULIAJI Ibrahima Fofana kutoka nchini Ivory Coast ametua nchini leo Jumanne mchana tayari kabisa kufanya majaribio ya kujiunga na Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC.
Mabingwa hao kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kukifanyia marekebisho kikosi chake na moja ya eneo walilolimulika ni kuboresha eneo la ushambuliaji kwa kusajili washambuliaji wapya wawili wenye viwango vya juu.
Fofana (26), ametua nchini akitokea timu ya Union Sportive de Ben Guerdane ya Tunisia aliyokuwa akiichezea msimu uliopita uliomalizika Juni 14 mwaka huu.
Nyota huyo mwenye uwezo wa kucheza namba 9, 7 na 11, kabla ya kujiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Tunisia (Ligue 1) alikuwa akikipiga kwa miamba ya Ivory Coast Asec Mimosas tokea mwaka 2013 hadi 2015.
Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya kutua, Fofana alisema nia yake kubwa ni kuisaidia Azam FC kwenda kimataifa zaidi endapo atafuzu majaribio hayo.
“Ninafuraha kabisa kukaribishwa na Azam FC, ni furaha yangu kuwepo hapa na nimekuja kuonyesha kipaji changu lakini pia kuisaidia timu kwenda kimataifa zaidi katika michuano mikubwa ya kimataifa, kwa hiyo nadhani timu wataweza kushuhudia kipaji changu na ni Mungu pekee ndiye ataisaidia nipite salama,” alisema.
Fofana ataanza rasmi majaribio yake keshokutwa Ijumaa kikosi cha Azam FC kitakapoendelea na mazoezi yake, ambapo kesho Alhamisi ni siku ya mapumziko.
Mshambuliaji huyo anaungana na makipa wawili wa kigeni, Daniel Yeboah (Ivory Coast) na Juan Jesus Gonzalez (Hispania), wanaoendelea kufanya majaribio ndani ya Azam FC wakigombea nafasi moja ya usajili ya golikipa.
0 Maoni:
Post a Comment