Friday, July 8, 2016

AZAM YAANZA MAZOEZI, KUCHEZA MECHI TANO ZA KIRAFIKI

Posted By: kj - 9:28 AM

Share

& Comment

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo imeanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya wa 2016-17.

Wachezaji wa kikosi hicho wameanza kujifua wakiwa chini ya benchi jipya la ufundi linaloongozwa na makocha kutoka nchini Hispania waliokuwa wakisaidiana na wazawa Kocha Msaidizi Dennis Kitambi na Daktari Juma Mwimbe.

Benchi hilo linaongozwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Msaidizi wake Yeray Romero, Kocha Mkuu wa Viungo Jonas Garcia na Msaidizi wake, Pablo Borges na Kocha wa Makipa Jose Garcia.

Katika mazoezi hayo ya kwanza makocha hao waliwapa mazoezi mengi ya kuuchezea mpira wachezaji kwa kugusa mpira mara mbili hadi tatu (2-3 touchs) pamoja na mazoezi mengi ya viungo ya kulainisha miili yao.

Baadhi ya nyota wa Azam FC waliohudhuria mazoezi hayo yaliyoanza saa 3.30 asubuhi ni nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na msaidizi wake Himid Mao ‘Ninja’, wengine ni kipa Aishi Manula, Farid Mussa, Erasto Nyoni, Frank Domayo.

Wengine walioongeza nguvu ni wachezaji wa kikosi hicho waliokuwa kwa mkopo msimu uliopita, viungo Omary Wayne na Bryson Raphael pamoja na mshambuliaji Kelvin Friday.

Pia kulikuwa na uwepo wa wachezaji kadhaa waliokuja kwenye majaribio wakiwemo makipa Daniel Yeboah (Ivory Coast), Juan Jesus Gonzalez (Hispania) na Nurdin Yusuf (Medeama, Ghana).

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuhusu programu waliyoaindaa kwa ajili ya kipindi hicho cha maandalizi ya msimu mpya (pre-season), Kocha Msaidizi Dennis Kitambi, alisema wameigawanya katika wiki sita.

“Katika wiki hii ya kwanza tutafanya mazoezi hadi Jumapili ijayo, kwa ujumla tmeigawanya katika wiki sita pre-season yetu, leo tumefanya mazoezi mara moja asubuhi na kesho tutafanya mara mbili asubuhi na jioni na kwa kumalizia Jumamosi na Jumapili tufanya mara moja kila siku,” alisema.


Wiki mbili kuamua majaribio


“Kuna wachezaji ambao wamekuja kwenye majaribio, tunategemea na wengine pia watakuja katika siku mbili tatu zijazo hiyo ni katika jitihada za timu kuboresha kikosi chake, tunategemea hao wachezaji wanaokuja tutapata kile tunachokitafuta.

“Hivi sasa ni mapema sana kuanza kusema viwango vyao kwani wamefanya mazoezi siku moja tu, kwa hiyo kadiri siku zitakavyokwenda tutaona nini wamefanya na mwisho wa siku ni jukumu la Kocha Mkuu Zeben  (Hernandez) kutoa uamuzi wake kuwa yupi amefuzu kwa takribani siku 15 au wiki mbili tunatarajia kujua hayo,” alisema.


Mechi tano za kirafiki


Kitambi aliendelea kusema kuwa katika programu hiyo wamepanga kucheza mechi za kirafiki zisizopungua tano ili kukipa makali kikosi hicho kabla hawajaanza msimu.

“Mechi ya kwanza ya kirafiki tunatarajia kucheza Julai 17, wiki nyingine inayofuata baada ya mchezo huo tunatarajia kucheza nyingine mbili na pia kuna  mkakati wa timu kwenda Visiwani Zanzibar kucheza mechi za kirafiki mbili kabla ya kurudi Dar es Salaam kufanya maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga,” alimalizia.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.