Saturday, July 2, 2016

KUMEKUCHA CHAMANZI, BENCHI LA UFUNDI LATUA, KUANZA KAZI JUMATATU

Posted By: kj - 11:00 PM

Share

& Comment

MAKOCHA wapya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC kutoka nchini Hispania, wametua rasmi jijini Dar es Salaam leo saa 9 Alasiri tayari kabisa kuanza maandalizi ya msimu ujao (2016-17).

Wakufunzi hao waliotua leo na kupokelewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, pamoja na Ofisa Habari Jaffar Idd, ni Kocha Mkuu Zeben Hernandez na Msaidizi wake Yeray Romero, Kocha Mkuu wa Viungo Jonas Garcia na Msaidizi wake, Pablo Borges na Kocha wa Makipa Jose Garcia.

Jopo hilo la makocha litaongezewa nguvu na makocha wengine wazawa waliokuwa na Azam FC msimu uliopita, Kocha Msaidizi Dennis Kitambi na wa Makipa, Idd Abubakar.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya kutua kwa mara ya pili nchini Kocha Mkuu Zeben, alisema wamekuja kuanza rasmi kazi kuanzia Jumatatu Ijayo (Julai 4, 2016) kwenye Makao Makuu ya Azam Complex, Chamazi.

Kocha huyo wa zamani wa CD Santa Ursula ya Hispania, alisema kuwa kabla ya kuanza kazi rasmi Jumatatu, kesho Jumapili wanatarajia kukutana na uongozi wa Azam FC pamoja na  kutembelea makao makuu ya Azam Complex.

Daktari kutua Julai 12


Katika hatua nyingine alisema kuwa Daktari wa timu hiyo, Sergio Perez, anatarajia kutua nchini Julai 12 mwaka huu, na hawakuweza kutua naye leo kutokana na kumalizia baadhi ya mambo na timu yake anayofanya kazi kwa sasa.

Tayari Zeben ameshaweka wazi kuwa jambo kubwa analokuja kulifanya Azam FC ni kuifanya timu hiyo ipate matokeo mazuri na kutisha barani Afrika ikiwa inacheza soka safi la kisasa lenye muoanekano wa Kihispania.  

C.E.O afafanua ujio wao


Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema kuwa makocha hao wanatarajia kuanza programu yao wiki ijayo huku kesho (Jumapili) wakitarajia kufanya nao kikao kwa ajili ya kujipanga na msimu ujao.

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu baada ya makocha wetu kufika salama, kama tulivyopanga kesho watakuwa na kikao na uongozi, baada ya hapo wataanza rasmi programu yao Jumatatu na hapo ndipo tutakuwa tunaanza maandalizi ya msimu ujao,” alisema.

Kucheza mechi za Kimataifa


Kawemba alisema kuwa katika maandalizi yao wamejipanga kuwatafutia makocha hao mechi za kirafiki za Kimataifa, endapo hakutakuwa na michuano ya Kombe la Kagame walilolitwaa mwaka jana kwa kuwachapa mabingwa wa Kenya Gor Mahia mabao 2-0.  

“Baada ya mazoezi hayo tunatarajia uwepo wa michuano ya Kombe la Kagame tukiwa mabingwa watetezi, kama haitakuwepo tumejipanga kutafuta mechi za kirafiki za Kimataifa kwa ajili ya kuiweka vizuri timu yetu kwa ajili ya msimu ujao na tunaamini ya kuwa utakuwa ni msimu wa mafanikio kwa upande wetu,” alisema.

Nyota wa kimataifa kutua


“Tunatarajia wiki ya kwanza ya mazoezi yetu watakaohudhuria watakuwa ni wachezaji wetu tuliokuwa nao msimu uliopita, ila tunatarajia kuwapokea wachezaji kadhaa wa kimataifa watakaokuja kwa majaribio hao wataanza kuingia nchini kuanzia Alhamisi ijayo na makocha wetu watatuambia ni wachezaji gani wanaowahitaji kuwasajili kwa msimu ujao,” alisema bosi huyo wa Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB.

Awatoa hofu mashabiki


Kutokana na Azam FC kuwa kimya kwenye zoezi la usajili linaloendelea hivi sasa, Ofisa huyo aliwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo na kuwaambia kuwa mambo mazuri yanakuja kuelekea msimu ujao.

“Tunawaomba mashabiki wa Azam FC wawe watulivu katika kipindi hiki, na nawaomba kwa wale wa karibu na Azam Complex wajitokeze kwa wingi kuanzia Jumatatu kushuhudia maandalizi yetu,” alisema.

Makocha hao wanatua nchini kuziba nafasi za benchi la ufundi lililopita la Azam FC chini ya Stewart Hall, Msaidizi wake Mario Marinica na Mtaalamu wa Viungo, Adrian Dobre, waliojiuzulu kuinoa timu hiyo mara baada ya mchezo dhidi ya JKT Ruvu (2-2) msimu uliopita.

Chanzo: azamfc.co.tz

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.