Friday, March 2, 2018

AZAM KUWAKABILI SINGIDA UNITED KESHO CHAMANZI

Posted By: kj - 11:21 PM

Share

& Comment

 
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa kibaruani kuvaana na Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jumamosi saa 1.00 usiku.

Mchezo huo unatarajia kuwa mkali na wa aina yake, ambapo kikosi cha Azam FC kipo tayari kwa ajili ya mtanange huo baada ya kufanya maandalizi makali ya wiki nzima kikiwa kimejipanga vilivyo kuzoa pointi zote tatu.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, mwanzoni mwa wiki hii aliweka wazi kuwa wanauchukulia kwa uzito mkubwa mchezo huo na watahakikisha wanaibuka na ushindi ili kujiweka sawa kwenye msimamo wa ligi.

“Lazima tuingie na tahadhari kwa sababu hatutaki kufungwa tunataka kushinda kwanza tunaweka usalama katika ulinzi wetu tuhakikishe mpira hauingii kwenye nyavu zetu halafu tutengeneze mipango ya kuhakikisha tunapata magoli ambayo yatatupa ushindi na pointi tatu ili tuzidi kuwavuka zaidi hao wapinzani wetu,” alisema.

Azam FC inatarajia kumkosa beki wake Yakubu Mohammed, ambaye bado ana maumivu ya mguu, huku wachezaji wengine watakaoukosa mchezo huo wakiwa ni beki Daniel Amoah, anayesumbuliwa na maumivu ya goti, mshambuliaji Wazir Junior na winga Joseph Kimwaga, wanaomalizia programu zao za kuuweka mwili sawa (recovery) kabla ya kuruhusiwa kucheza mechi ya ushindani.

Huo utakuwa mchezo wa tatu kwa timu hizo kukutana msimu huu, mchezo wa kwanza ulikuwa ni wa ligi ulioisha kwa sare ya bao 1-1, Azam FC ikijipatia bao lake kupitia kwa kinda Paul Peter huku Singida ikitangulia kufunga kupitia kwa Danny Usengimana.

Mchezo wa pili kwa timu hizo kukutana ulikuwa ni wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu na Azam FC kushinda bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Shaaban Idd, lililowahakikishia kutwaa ubingwa huo kwenye fainali kwa kuifunga URA ya Uganda.

Timu hizo zitaingia kwenye mchezo huo, zikitoka kupata sare kwenye mechi zao zilizopita za ligi, Azam FC ikipata suluhu dhidi ya Lipuli huku Singida ikitoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar, mtanange uliofanyika Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, Kagera.

Hadi sasa timu hizo zinafukuzana kwa ukaribu kwenye msimamo, Azam FC ikishika nafasi ya tatu kwa pointi 35, Singida ikiwa ya nne kwa pointi 34, timu mbili za juu zikiwa ni Simba yenye pointi 46, Yanga ikifuatia nafasi ya pili na pointi zake 40.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.