Sunday, October 8, 2017

Kuelekea mchezo wa Mwadui vs Azam FC

Posted By: kj - 5:28 PM

Share

& Comment

IMEBAKI wiki moja kabla ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, haijaivaa Mwadui katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inayotarajia kufanyika Oktoba 14 mwaka huu.

Ili kujipanga vilivyo na mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam keshokutwa Jumanne alfajiri kuelekea mkoani Shinyanga tayari kabisa kuikabili Mwadui kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Azam FC inauchukulia uzito mchezo huo na katika mikakati ya kuhakikisha inafanya vizuri, kikosi hicho kimepanga kuondoka na wachezaji wote iliowasajili msimu huu ambao wako fiti.

Baada ya kikosi hicho kucheza na Mwadui, kinatarajia kusalia Kanda ya Ziwa ili kufanya maandalizi ya mchezo mwingine wa ugenini dhidi ya Mbao, unaotarajia kufanyika mkoani Mwanza Oktoba 21 mwaka huu, ambao utahitimisha siku 12 za Azam FC katika mikoa hiyo miwili ya kanda hiyo.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita wanaodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora nchini ya NMB na Tradegents, wanaelekea kucheza mechi hizo wakiwa na rekodi bora kabisa ndani ya ligi hiyo ikiwa ni miongoni mwa timu tatu za juu kileleni.

Timu hiyo ipo juu baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 11 sawa na Simba na Mtibwa Sugar zilizo juu yake kwa tofauti ya mabao ya kufunga, lakini Azam FC inabakia kuwa ndio timu pekee iliyofungwa bao moja pekee katika mechi tano za ligi zilizochezwa mpaka sasa.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.