Thursday, March 8, 2018

AZAM WAICHAPA MWADUI NAKUSOGEA MPAKA NAFASI YA PILI

Posted By: dada - 10:30 PM

Share

& Comment

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya kweli baada ya kuidungua Mwadui bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliomalizika Uwanja wa Azam Complex usiku huu.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha jumla ya pointi 41 na kuishusha Yanga yenye mechi mbili mkononi hadi nafasi ya tatu ikibakiwa na pointi zao 40 huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 46.

Bao pekee la Azam FC limewekwa kimiani na mshambuliaji Yahya Zayd, dakika ya tano akitumia uzembe wa kipa wa Mwadui, Anold Massawe, aliyepiga mpira vibaya na kumpasia mguuni mfungaji wakati akiwa kwenye harakati za kuupiga mbele mpira aliorudishiwa na beki wake, Idd Mfaume.

Kama Zayd angekuwa makini huenda angeipatia mabao zaidi Azam FC baada ya kupoteza takribani nafasi nne za kufunga huku wengine waliokosa nafasi wakiwa ni Shaaban Idd na Bernard Arthur, walioingia kwa nyakati tofauti kuchukua nafasi za Mbaraka Yusuph aliyeumia na Frank Domayo.

Nyota wa mchezo huo kwa upande wa Azam FC, alikuwa ni kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, aliyefanikiwa kupiga pasi nyingi za hatari na kuichezesha timu kwa asilimia kubwa.’

Dakika ya 75, ilishuhudiwa nahodha wa Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, akiingia uwanjani kuchukua nafasi ya Shaaban, ikiwa ni mechi yake ya kwanza tokea akae nje ya dimba kwa takribani wiki sita akiuguza majeraha ya chini ya goti kwenye ugoko, ambapo mchezo wa mwisho kucheza ulikuwa dhidi ya Yanga Januari 27 mwaka huu.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuendelea na mazoezi kesho Ijumaa jioni kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Mbao unaotarajia kufanyika Uwanja wa Azam Complex Jumapili hii saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC:

Mwadini Ally, David Mwantika, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Agrey Moris, Salmin Hoza, Salum Abubakar, Frank Domayo/Arthur dk 82, Yahya Zayd, Mbaraka Yusuph/Shaaban/Himid dk 24,75, Joseph Mahundi

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.