Friday, March 9, 2018

AZAM FC YAJIAANDA KUIMALIZA MBAO FC

Posted By: dada - 12:00 PM

Share

& Comment

MARA baada ya kuvuna pointi tatu dhidi ya Mwadui usiku wa kuamkia leo, benchi la ufundi la Azam FC hivi sasa linaandaa mbinu za kuiua Mbao katika mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex keshokutwa Jumapili saa 1.00 usiku.

Bao pekee la Azam FC usiku wa jana limefungwa na mshambuliaji Yahya Zayd, aliyetumia uzembe wa kipa wa Mwadui, Anold Massawe, ushindi ulioifanya kupanda hadi nafasi ya pili ikifikisha pointi 41ikiiacha Yanga yenye mechi mbili mkononi iliyodondokea nafasi ya tatu kwa pointi 40 huku Simba ikiwa kileleni na pointi zake 46.

“Mbao ni timu nzuri hasa ikicheza na timu kubwa wanakuwa wazuri na sisi tutajiandaa tutaangalia mechi zao kuona jinsi gani wanavyocheza, tunawajua Mbao walivyo lakini tutazidi kuwaangalia ili tutengeneze mfumo ambao tunajua tunaweza kuwadhibiti kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz

Aidha akizungumzia mchezo uliopita dhidi ya Mwadui, Cheche alisema wanashukuru kuweza kuibuka na ushindi licha ya kutokuwa mrahisi huku akidai watafafanyia kazi tatizo la kukosa mabao lililoonekana kwa kiasi kikubwa kwa upande wao na kushindwa kupata ushindi mnono.

“Wachezaji wetu kidogo waliwachukulia kawaida Mwadui, lakini Mwadui walikuwa wako wazuri walijaribu kushambulia lakini kikubwa katika mchezo huu tumepata nafasi nyingi tumekosa kuwa makini katika umaliziaji.

“Naona lile tatizo ambalo lilikuwa limeshaanza kutoka linajirudia tena itabidi tuanze kupambana nalo kuhakikisha nafasi tunazozipata tunajaribu kuzitumia kwa asilimia 80, wachezaji wetu toka wanaanza walikuwa wapo chini nafikiri waliiona Mwadui kama ni timu dhaifu wakati katika ligi timu zote ni nzuri huwezi kuidharau timu hilo limetufanya kuwa chini kidogo na tumepoteza nafasi nyingi,” alisema.

Mabingwa hao wa ligi msimu wa 2013/2014, wanatarajia kuanza mazoezi ya kujiandaa na mchezo ujao leo Ijumaa jioni kwenye viunga vyake vya Azam Complex, wakiwa na uchu mkubwa wa kuendeleza wimbi la ushindi na kuzidi kufukuzia ubingwa wa ligi hiyo.

Katika mchezo wa raundi ya kwanza timu hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ziliweza kutoka suluhu.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.