VIUNGO wawili tegemeo wa
Azam FC na ambao hivi sasa wako juu ile mbaya kimchezo, Ibrahim Mwaipopo
na Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’ sasa wanaendelea vizuri na kuna
matumaini wakawa fiti kwa mechi ya Ngao ya Jamii, Septemba 11 dhidi ya
Simba, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viungo hao wamekwishaanza
mazoezi mepesi, wakiongozwa na daktari wa timu hiyo, Dk Mwanandi
Mwankemwa kuanzia gym hadi uwanjani. Dk. Mwanandi anasema wachezaji hao
hali zao zinatia matumaini kwa sasa na wataendelea kuwaangalia hadi
mwishoni mwa wiki ili kujua maendeleo yao.
Viungo hao tegemeo
hakuwemo kwenye mechi ya kirafiki Jumapili dhidi ya Coastal Union ya
Tanga, kwenye Uwanja wa Chamazi, kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Simba.
Katika mechi hiyo
iliyokuwa tamu, mabao mawili ya John Raphael Bocco ‘Adebayor’ katika
dakika za 15 na 44, yaliipa Azam FC ushindi wa mabao 2-0 Uwanja wa
Chamazi.
Bocco alikuwa mwiba
mchungu kweli siku hiyo kwa safu ya ulinzi ya Coastal, kwani pamoja
kufunga mawili, lakini alikosa mabao matatu ya wazi mno katika mechi
ambayo, kiungo Abdulhalim Humud alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika
ya 32 kwa rafu na lugha chafu.
Hiyo ni mechi ya tano
Coastal inafungwa kati ya sita za kujipima nguvu ilizocheza kabla ya
Jumamosi kufungwa 2-1 na Yanga, awali ilifungwa 3-2 na Bandari mjini
Mombassa, baadaye 2-0 Tanga, ilifungwa 2-1 na Polisi mjini Morogoro na
yenyewe iliifunga JKT Oljoro 1-0.
Kwa Azam hiyo ni mechi ya
tatu mfululizo ya kujipima nguvu wanashinda, awali walizifunga 1-0
Prisons ya Mbeya na Transit Camp 8-0.
Azam inatarajiwa kuivaa
Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia
la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo wake wa kwanza katika historia ya
Ngao hiyo.
Kihistoria hiyo itakuwa
mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha
timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga
mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao,
wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado
inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari
Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga
ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena
Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa
Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe mara ya mwisho
Simba SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita Dar es Salaam,
ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na Bocco na lile la kufutia machozi
kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na beki mahiri Shomari
Kapombe, aliyemajeruhi kwa sasa.
0 Maoni:
Post a Comment