KLABU ya Azam FC kwa sasa imeingia vitani kusaka wachezaji wawili kuongeza nguvu katika nafasi ya winga pamoja na kiungo.
Awali klabu hiyo ilitaka kumsajili kiungo wa
zamani wa Yanga, Athumani Idd ‘Chuji’ lakini waliamua kuachana na mpango
huo kutokana na rekodi mbaya ya nidhamu ya mchezaji huyo.
Azam imepania kupata kiungo huyo kwa sasa hasa
baada ya kuumia kwa kiungo wao mpya Frank Domayo aliyefanyiwa operesheni
ya nyama za paja na atakaa nje ya uwanja kwa miezi tisa.
Wakizungumza na Mwanaspoti, Kocha mkuu wa timu
hiyo, Joseph Omog na meneja wa timu hiyo, Jemedari Said wamesema tayari
uongozi wa klabu hiyo umebariki mpango huo, hivyo kwa sasa wanaangalia
wachezaji wanaokidhi mahitaji yao kwa sasa.
“Tumependekeza kwa uongozi kuongezewa nguvu ya
wachezaji wawili, mmoja atakuwa ni kiungo na mwingine ni winga, hilo
linabidi kufanyika katika majira haya ya usajili na mpaka sasa wapo
baadhi ya wachezaji tunaowahitaji,” alisema Omog.
Meneja wa timu hiyo, Jemedari alisema kuwa “Muda
wa usajili bado upo hivyo tutafanya kwa umakini zaidi ili kuwapata
wachezaji hao watakaotufaa,”.
Wakati huohuo, Omog alisema kuwa kuanzia wiki hii
kikosi chake kitaanza kucheza mechi za kirafiki mara mbili kwa wiki
ambapo leo Jumanne asubuhi Azam watacheza na Polisi Moro iliyopanda
daraja, mechi hiyo itachezwa Chamazi.
“Wachezaji wanaendelea vizuri, wameonyesha ukomavu
mzuri kwa sasa tumepanga kuwa na mechi mbili za kirafiki kila wiki ili
tuweze kuona sehemu zenye upungufu na kuziboresha zaidi.” alisema Omog.
CHANZO: MWANASPOTI
0 Maoni:
Post a Comment