Wednesday, December 24, 2014

NKAMIA AIPONGEZA AZAM FC

Posted By: kj - 6:28 AM

Share

& Comment

http://shaffihdauda.co.tz/wp-content/uploads/2014/12/jk.png
NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia ameipongeza klabu ya soka ya Azam kwa kufanikisha mpango wa kuzindua kadi kwa mashabiki wao kwa kushirikiana na wafadhili wao wakuu benki ya NMB.

Katika hafla hiyo iliyofanyika makao makuu ya klabu hiyo Chamazi, Nkamia aliwataka mashabiki hao kuipa sapoti timu hiyo ili izidi kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakayoshiriki mapema mwakani.

“Faida kubwa ya mashabiki duniani ni kuishangilia timu yao na kuizomea timu pinzani lengo ni kuwatia moyo wachezaji wa timu yao ili iweze kufanya vizuri ndani na nje ya Tanzania wakishirikiana na wadhamini wao NMB,” alisema Nkamia.
Nkamia aliipongeza Azam kwa kuanzisha utaratibu huo wa kutoa kadi za kuwatambua mashabiki wao, lakini ameitaka NMB kuhakikisha inasambaza utaratibu huo mikoani ili uweze kuwafikia wapenzi waliopo nje ya Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Fedha wa NMB, Wazir Barnabas, alisema maamuzi hayo ya kutengeneza kadi kwa mashabiki wa Azam ni makubaliano ya pande zote mbili kwa lengo la kuiongezea timu hiyo mashabiki wa kutosha.

“Haya ni makubaliano ya pande zote mbili yani Azam na NMB, lengo ni kuona Azam inakuwa na hazina kubwa ya mashabiki ambao katika mchezo wa soka ni watu muhimu katika kuchangia mafanikio na ushindi wa timu,” alisema Barnabas.

Barnabas alisema shabiki yeyote wa Azam atakayefanikiwa kupata kadi hiyo itamfanya kuwa mteja wa NMB atakayeweza kupata huduma zote ikiwemo kutoa pesa katika mashine za ATM kokote nchini.

Kwa kuanzia NMB imetoa kadi 100 na kwa mujibu wa Mwenyekiti wa timu hiyo Said Mohamed, huduma hiyo itakuwa ikiendelea kadri siku zinavyokwenda ili ziweze kumfikia kila shabiki ambaye atajiandikisha na kufuata maelekezo yanaho hitajika.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.