Tuesday, February 3, 2015

OMOG BADO ANA MIAKA 3

Posted By: Unknown - 10:06 PM

Share

& Comment

KAMA ulikuwa unajidanganya kuwa Azam itamtimua kocha wake, Joseph Omog, ndani ya mwaka huu ama mwaka ujao ujue unajidanganya kwani mabosi wa timu hiyo wameamua kumpa miaka mitatu ya kutengeneza timu.

Omog amekuwa akikosolewa kwa kushindwa kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri kwa kutocheza kandanda safi kulingana na aina ya wachezaji alio nao, lakini mabosi wa timu hiyo wameamua kumpa muda wa kulitimiza hilo.

Habari kutoka chanzo cha kuaminika ndani ya Azam zinaeleza kuwa mabosi wenye maamuzi ya juu ya timu wameamua kwa kauli moja kumwacha Omog afanye kazi yake kwa muda wa miaka mitatu ndipo waamue kama anaweza kuendelea ama la.

"Kulikuwa na chokochoko nyingi wakati tumeondolewa kwenye Kombe la Mapinduzi, kuna baadhi ya wachezaji walisema kocha ameishindwa timu na kutaka aondoke, lakini mabosi wakaweka ngumu," kilisema chanzo chetu hicho.

"Hapa Omog hawezi kuondoka kwani mabosi wamesema wanampa miaka mitatu atengeneze timu yenye uwezo wa kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika.

"Kuna baadhi ya wachezaji walishaanza mgomo baridi kutaka kocha aondoke, lakini wakaambiwa kuwa wataondolewa wao na hivyo kuamua kuachana na mambo hayo na kuanza kucheza kwa kujituma."

Omog amesema aina ya uchezaji ya mshambuliaji wa timu hiyo, Kipre Tchetche ni kama Cristiano Ronaldo hivyo hawezi kusaidia timu katika kukaba kama inavyotarajiwa na wengi. Tchetche amekuwa akilaumiwa kwa kushindwa kurudi kusaidia kukaba pale timu inapopoteza mpira na kusababisha timu pinzani kupitia winga yake kwa muda mwingi wa mchezo na kumfanya beki wa kushoto wa timu hiyo kushindwa kupanda.

"Kipre Tchetche anacheza kama Ronaldo, ni mzuri katika mashambulizi lakini kukaba kwake ni shida, ni tatizo dogo la kufanyia kazi lakini siyo sababu ya kumweka benchi," alisema Omog.

"Pia kwa sasa bado Tchetche hajawa fiti asilimia zote, kumbuka alitoka kwenye majeruhi katikati ya mwezi uliopita na bado anajitahidi kujijenga."


chanzo: mwanaspoti

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.