Monday, August 17, 2015

MAKALA: AZAM IMEPANIA KINOMA

Posted By: kj - 12:58 PM

Share

& Comment

AZAM ndiyo timu tajiri zaidi nchini unapozungumzia suala la uwekezaji katika soka uliofanywa na klabu hiyo. Simba na Yanga hizo zina utajiri wa watu ambao hata hivyo wameshindwa kutumika vizuri kuleta maendeleo ya klabu.

Azam ina kiwanja kizuri cha mazoezi na mechi, gym, hosteli, magari ya kisasa na vitu vingine kadhaa muhimu katika timu. Ni tofauti sana na unaposema klabu ya Simba ama Yanga ambazo utazungumzia majengo na watu pamoja na porojo za ujenzi wa viwanja vyao.

Mbali na rasilimali hizo Azam pia inaendeshwa kisomi, kila kitu kinakwenda kimpangilio na sasa wanafurahisha zaidi, mfano kama jambo lipo kwenye mipango yao halafu mmoja wao akajifanya kulitoa kabla halijakamilika basi mpango huo hufutwa kabisa ili kutengeneza heshima katika uongozi.

Timu hiyo imepiga kambi visiwani Zanzibar na inatarajia kurejea jijini Dar es Salaam wiki hii ikiwa tayari imeiva kucheza na Yanga katika mechi ya Ngao ya Hisani Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga hiyo imejichimbia mkoani Mbeya.

Mchezo huo unatajwa kuwa wa kisasi kutokana na Azam kuiondoa Yanga katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Kagame mwezi uliopita.

Mwanaspoti liliibuka katika kambi ya timu hiyo ambayo ilipigwa katika hoteli ya kitalii ya Zanzibar Ocean View na kushuhudia mazoezi na maisha ya timu hiyo.

Ratiba ya mazoezi


Kocha mkuu wa Azam, Stewart Hall anasema amepanga ratiba ambayo si ya kuwachosha wachezaji wake kwani anataka zaidi akili zao zitulie kwa ajili ya mechi ijayo, hataki wacheze kwa jazba ili kupata matokeo mazuri na ndiyo maana amewaficha visiwani hapa.

“Huwa tunafanya mazoezi mara mbili kwa siku ila kama asubuhi nafanya kwa muda mrefu uwanjani basi jioni nawapeleka ufukweni kwa ajili ya mazoezi ya kuifanya miili yao iwe na nguvu kwani uwanjani nafundisha jinsi ya kuchezea mpira na mbinu nyingine.

“Hata hivyo ufukweni huwa situmii muda mwingi, natumia saa moja tu inatosha kwani naamini kikosi changu bado ni imara na kitafanya vyema katika michuano yote iliyopo mbele yetu.”

Mapumziko


Kila baada ya mechi ya kirafiki Hall hutoa mapumziko kwa wachezaji lakini mapumziko hayo ni baada ya kutoka ufukweni ambako yeye anaamini mchezaji ukimpeleka sehemu kama hizo akili yake hukaa sawa.

“Baada ya mechi na KMKM kesho yake niliwapeleka ufukweni kwa muda mfupi tu na jioni niliwaruhusu watoke, na hata baada ya mechi yetu na Mafunzo napo niliwaacha huru ila baada ya kutoka ufukweni asubuhi, nafanya hivyo kujaribu kucheza na saikolojia zao ili wasijione kama wafungwa.”

Msosi wa maana


Hall anasema mchezaji anatakiwa kuwa na mlo uliokamilika na anatakiwa kula kwa wakati unaostahili, yeye anaelezea “Nimerudi Azam na nimebadilisha baadhi ya mambo kwa wachezaji ikiwemo mlo, mchezaji hawezi akawa anajilia tu chakula bila kuzingatia ni chakula gani anapaswa kula na kwa wakati upi,”.

Kutokana na hilo Azam imekuwa ikipata chakula kulingana na ratiba ya mazoezi ya siku husika pamoja na maelekezo kutoka kwa kocha na daktari wa timu hiyo.

Kikosi ngangari


Ukiiangaia timu ya Azam FC huwezi kugundua mara moja kwamba hiki ndiyo kikosi cha kwanza tofauti na Simba na Yanga ambazo kabla hata ya mechi unaweza kujua nani anacheza kikosi cha kwanza na nani anakuwa benchi.

“Timu yangu yote ni nzuri, siwezi kusema nani ni kikosi cha kwanza ama cha pili, ndiyo maana naweza kuchezesha mchezaji yeyote na akafanya vizuri, kwa sasa sitaki wapinzani wakariri nani anaanza nani ataingia. “Kuna baadhi ya wachezaji nawafundisha kucheza nafasi tofauti na walizozoea akiwemo Ramadhan Singano ‘Messi’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Ame Ally, hivyo mtu anaweza kujiuliza kwanini nawabadilisha ila ni kuwaondolea mazoea wapinzani wetu,” anasema Hall.

Messi na Sure Boy anawafundisha kucheza kama washambuliaji wa kati wakati Ame ambaye ni straika huwa anacheza kama kiungo mkabaji.

Nidhamu


“Nafurahishwa na nidhamu ya wachezaji wawapo nje ya uwanja na ndani ya uwanja, wananiheshimu na ninawaheshimu pia, sitaki kuona mchezaji mmoja anakuwa mnyonge katika kikosi changu kisa ananiogopa, ila nataka mchezaji ajitambue na ajitume zaidi kwani hii ni kazi yake.”

Familia moja


Hakuna sehemu ambayo kuna mkusanyiko wa watu na isiyokuwa na makundi.Hali hiyo ni ya kawaida sana hata kwenye timu hizi za soka makundi yapo lakini je nani wa kuyafanya makundi hayo yakiwepo yasiwe na madhara kwa timu husika? “Hilo ni jukumu langu kama kocha, kwani mimi ndiye mlezi wa wachezaji, niliporudi kuna mambo niliyakuta lakini nashukuru nimeweza kuyaondoa kwa asilimia kubwa.”

IMETOLEWA NA: MWANASPOTI

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.