Sunday, April 24, 2016

AZAM FC YATINGA FAINALI YA KOMBE LA TFF

Posted By: kj - 11:30 PM

Share

& Comment


KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imetinga fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya jioni ya leo kuichapa Mwadui ya Shinyanga kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia sare ya mabao 2-2 hadi dakika 120 zilipomalizika.

Shujaa wa Azam FC kwenye mchezo huo alikuwa ni kipa Aishi Manula aliyeupangua kiustadi mkwaju wa nne wa penalti wa Mwadui uliopigwa na mshambuliaji Kelvin Sabato na beki Aggrey Morris kufunga mkwaju wa tano wa penalti ulioipeleka timu hiyo fainali.

Azam FC ilianza mchezo huo kwa kasi ikitafuta bao la mapema na hatimaye ikapata bao la uongozi dakika ya tatu lililofungwa na mshambuliaji Khamis Mcha kwa shuti zuri la kiufundi nje kidogo ya eneo la 18 kufuatia krosi ya beki Erasto Nyoni na shuti hilo kumshinda kipa wa Mwadui, Shaaban Kado.

Baada ya kuingia bao hilo Mwadui iliamka na kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Azam FC, lakini umwamba wa kipa Aishi Manula ulimnyima nafasi mbili za wazi mshambuliaji Kelvin Sabato baada ya kipa huyo kuokoa michomo yake na kufanya kipindi cha kwanza kimalizike kwa mabingwa hao kuongoza kwa bao hilo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kufanya mabadiliko ya kuingia kiungo Frank Domayo na kutoka Ramadhan Singano ‘Messi’, mabadiliko ambayo yaliiongezea kasi kwa timu hiyo kusaka bao la pili kabla ya kiungo huyo kucheza akiwa anachechemea kwa takribani dakika 25 za mwisho za kipindi hicho baada ya kuumia mguu huku nafasi za wachezaji wa akiba zikiwa zimeshatumika zote.

Mwadui iliweza kusawazisha bao hilo dakika ya 82 kupitia kwa Salum Kabunda aliyepiga shuti kali lililogonga mwamba wa juu na kuingia ndani na hivyo kufanya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kufuatia muda wa kawaida wa mchezo kumalizika kwa timu hizo kwenda sare, ilibidi ziongezwe dakika 30 za nyongeza kwa mujibu wa kanuni za michuano hiyo ili apatikane bingwa atakayetinga hatua ya fainali.

Alikuwa ni Mcha tena dakika ya 97 aliyeipatia Azam FC bao la pili kwa shuti zuri baada ya kuwatoka walinzi watatu wa Mwadui karibu na eneo la kibendera kwa kuwahadaa na kuingia na mpira ndani ya eneo la 18 kisha kupiga shuti lilimpita kipa Kado na kupenya kujaa wavuni.

Hilo ni bao la tatu la Mcha msimu huu, yote akifunga kwenye michuano hiyo, moja jingine alitupia wakati Azam FC ilipoichapa Tanzania Prisons mabao 3-1 na kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.

Baada ya dakika 120 kumalizika mwamuzi wa mezani aliongeza dakika tatu za nyongeza, lakini cha kustaajabisha mara baada ya kuisha dakika hizo mwamuzi wa mchezo huo Andrew Shamba alitoa penalti ya kushangaza akidai kuwa Wazir Salum alishika mpira ndani ya eneo la 18, kumbe mpira huo ulimgonga juu ya paja na kuokoa.

Mwamuzi huyo alifikia hatua ya kumwonyesha kadi nyekundu beki wa Azam FC, David Mwantika na hivyo kuifanya timu hiyo kumaliza mchezo huo wakiwa pungufu, penalti hiyo ilifungwa vema na kiungo wa zamani wa matajiri hao, Jabir Aziz ‘Stima’ na kuisawazishia timu yake.

Hadi dakika 120 za mchezo huo zinamalizika timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 na hivyo kulazimisha mechi hiyo iamuriwe kwa changamoto ya kupigiana mikwaju ya penalti.

Azam FC ilipata penalti zote tano walizopiga zilizofungwa vema na Wazir Salum, Allan Wanga, Himid Mao, John Bocco na beki Aggrey Morri aliyefunga ya ushindi, huku Mwadui ikitupia tatu zilizopigwa na Jabir Azizi, Idd Moby, Malika Ndeule na ya nne iliyopigwa na Kelvin Sabato iliota mbawa kwa kupanguliwa na Aishi Manula.

Azam FC yaandika rekodi

Kuingia huko fainali kwa Azam FC kunaifanya kuandika rekodi ya kutinga fainali ya kwanza ya michuano hiyo, ambayo imerejeshwa mwaka huu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kukosekana kwa takribani miaka 14.

Sasa Azam FC inasubiria kutangazwa mshindi wa nusu fainali nyingine iliyovunjika dakika ya 110, ambayo ilizikutanisha wenyeji Coastal Union na Yanga katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Nusu fainali hiyo imevunjika baada ya kutokea vurugu kubwa ya mashabiki wakipinga maamuzi ya mwamuzi Abdallah Kambuzi, wakati huo Yanga ikiongoza mabao 2-1.

Fainali ya michuano hiyo inatarajia kufanyika Mei 25 mwaka huu na bingwa ataiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.