KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, itaanza kutetea ubingwa wake wa Kombe la Kagame kuanzia Julai 16 hadi 30 mwaka huu, michuano itakayofanyika jijini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya pili mfululizo michuano hiyo inafanyika Dar es Salaam, ambapo mwaka jana Azam FC iliutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza kihistoria baada ya kuwachapa mabingwa wa Kenya Gor Mahia kwa mabao 2-0.
Tayari uongozi wa Azam FC umepokea barua rasmi kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao ndio waandaaji kwa mara nyingine, juu ya ufanyikaji wa michuano hiyo, ambayo awali ilipangwa kupigwa visiwani Zanzibar.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, iliweza kuifikia rekodi ya klabu kongwe ya SC Villa ya Uganda waliyoiweka mwaka 2005 baada ya kutwaa ubingwa huo kwa staili ya kipekee kwa kushinda mechi zote na kutofungwa bao lolote ndani ya dakika 90.
Villa nao waliweka rekodi hiyo ndani ya ardhi ya Tanzania kama walivyofanya wenyeji Azam FC, ambao wanaingia kwenye michuano hiyo mwaka huu kupitia nafasi ya kuwa bingwa mtetezi.
0 Maoni:
Post a Comment