Sunday, May 8, 2016

AZAM YAICHAPA KAGERA SUGAR GOLI 2

Posted By: kj - 8:56 PM

Share

& Comment

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imerejea nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga jioni ya leo.

Huo ni ushindi wa kwanza kwa Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB baada ya kuambulia sare mbili kwenye mechi mbili zilizopita na ikapoteza nafasi yake ya pili baada ya kupoomywa pointi tatu na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) katikati ya wiki hii.

Azam FC imerejea tena nafasi hiyo baada ya kufikisha jumla ya pointi 60 na kuwashusha
wapinzani wao Simba waliofungwa bao 1-0 na Mwadui ya Shinyanga leo katika Uwanja wa Taifa, lakini wakiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex,

Matokeo hayo ya Simba yameipa rasmi ubingwa wa ligi hiyo Yanga leo yenye pointi 68 kwani haitaweza kuzifikia pointi hizo walizofikisha hata kama itashinda mechi zake tatu zilizobakia kwani watafikisha 67.

Wakati Azam FC ikipanda juu, matokeo hayo yamezidi kuiweka pabaya Kagera Sugar kwenye vita ya kupigania kutoshuka daraja kwani wakiwa na pointi zao 25 katika nafasi ya 14 inatakiwa kushinda mechi zake zote mbili zilizobakia ili kujihakikishia kubakia Ligi Kuu msimu ujao.

Walikuwa ni Kagera Sugar walioanza kupata bao la uongozi dakika ya 24 kupitia kwa winga wao hatari upande wa kushoto, Adam Kingwande, aliyetumia vema uzembe wa safu ya ulinzi ya Azam FC.

Wachezaji wa Azam FC walijitahidi kurejea mchezoni, lakini walishindwa kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri ya kiuchezaji kwenye eneo la ushambuliaji na kiungo na hivyo kufanya bao hilo lidumu hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika.

Mabadiliko yaliyofanywa kabla ya kuanza kipindi cha pili na benchi la ufundi la Azam FC la kumuingiza mshambuliaji chipukizi aliyepandishwa msimu huu, Shaaban Idd na kumpumzisha Ame Ally, yalileta uhai kwenye eneo la ushambuliaji.

Hatimaye dakika ya kwanza tu ya kipindi cha pili kinda huyo akasababisha bao la kusawazisha la Azam FC baada ya kupiga kichwa kilichokwenda kwa Khamis Mcha aliyempasia Kipre Tchetche na kufunga bao hilo.

Azam FC ilizidi kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Kagera Sugar ili kupata bao la ushindi na hatimaye dakika ya 59 juhudi binafsi alizofanya nahodha wa timu hiyo leo, Himid Mao ‘Ninja’, ziliweza kuipatia bao la ushindi baada ya kupiga shuti kali umbali wa takribani mita 30 lililomshinda kipa wa Kagera Sugar, Agathony Anthony na kujaa wavuni.

Hilo linakuwa bao la kwanza kwa nahodha msaidizi huyo wa kikosi hicho msimu huu, ambaye alitengeneza mabao yote mawili ya Azam FC katika mchezo uliopita dhidi ya JKT Ruvu ulioisha kwa sare ya mabao 2-2.

Kwa mujibu wa takwimu za mchezo huo, Azam FC ilionekana kucheza vema zaidi kipindi cha pili tofauti na ilivyoanza kipindi cha kwanza, jambo ambalo liliweza kufanya waondoke na pointi zote tatu huku shukrani za pekee zimwendee kipa Aishi Manula, aliyeokoa michomo kadhaa ya washambuliaji wa Kagera Sugar, Kingwande na Daudi Jumanne.

Mara baada ya mchezo huo, Azam FC itaanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho saa 6 mchana ikitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa mkoani Mwanza kabla ya kuanza maandalizi ya kujiandaa na mechi mbili za mwisho za ligi dhidi ya African Sports (Mei 15, Mkwakwani) na Mgambo JKT (Mei 21, Azam Complex).

Vikosi vilivyocheza:

Azam FC; Aishi Manula, Gadiel Michael, Abdallah Kheri, Aggrey Morris, David Mwantika, Michael Bolou, Ame Ally/Shaaban Idd dk 46, Didier Kavumbagu/Allan Wanga dk 73, Himid Mao (C), Kipre Tchetche, Khamis Mcha/Ramadhan Singano dk 81

Kagera Sugar; Agathon Anthony, Ibrahim Job/Salum Kanoni dk 64, Juma Jabu, Erick Kyaruzi, Shaban Ibrahim, George Kavila, Juma Mpola/Paul Ngalyoma dk 82, Babu Ally, Mbaraka Yusuph, Adam Kingwande, Daudi Jumanne

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.